SHIRIKA la Huduma kwa Wanyamapori nchini (KWS) limezidisha hamasa kwa jamii zinazoishi vijijini Lamu kuepusha migogoro na wanyamapori huku ukame ukiendelea kukithiri eneo hilo. Mkurugenzi wa KWS Kaunti ya Lamu Ibrahim Ahmed, amesema shirika hilo pia limeweka mikakati ili kuhakikisha wanyamapori wanasambaziwa maji porini endapo kiangazi kitaendelea, ili kuwazuia kuingia vijijini. “Kuna mabwawa machache msituni ambayo bado yana maji ya kuwatuliza wanyamapori msimu huu wa kiangazi ila yapo kwenye hatari ya kukauka. Tumejiandaa. Endapo kutakuwa na haja tutawasambazia wanyamapori maji ili wasifike vijijini na kusababisha majeruhi au maafa,” akasema Bw Ahmed. Aliwashauri wananchi kuepuka kuvamia misitu ambayo ni makazi ya wanyama na kuigeuza kuwa sehemu za kuishi binadamu. Kauli ya afisa huyo inajiri wakati ambapo serikali ya kaunti tayari imeanzisha mpango kuwasambazia maji wakazi wa vijiji vyote vinavyoshuhudia makali ya ukame kote Lamu. Gavana wa Lamu Issa Timamy pia ametangaza kwamba serikali yake imetenga bajeti maalum ya kushughulikia athari za kiangazi. “Tumeanza kusambaza maji kupitia malori na mashua maeneo kama Witu, Pandanguo, Bar’goni, Kiangwe na kwingineko. Ukame unaendelea kuenea na lazima tusaidie watu wetu. Pia kaunti imetenga fedha za bajeti ya muda itakayoshughulikia makali ya ukame,” akasema Bw Timamy. Wakati huo huo, Bw Timamy amewahimiza wasichana wazidi kutia bidii masomoni ili wapate fursa za ajira wanazotengewa wanawake katika serikali ya kaunti. Gavana huyo amesema kihistoria, Lamu imekuwa nyuma katika kuwajumuisha wanawake uongozini lakini hali hiyo imebadilika. Kulingana naye, jinsia ya kike imepewa kipaumbele kwenye nyadhifa mbalimbali za uongozi katika serikali ya kaunti na pia ile ya kitaifa. Kikatiba, serikali huhitajika kuhakikisha kuna usawa wa kijinsia katika ajira zinazotolewa kwa umma. Lamu ina mawaziri saba ambapo kati yao, wanne ni wanawake. “Akina dada wana bidii na hujitolea. Utapata hata wakati wa kupigakura wanawake ndio hujitokeza kwa wingi,” akasema Bw Timamy. Mawaziri wa kike wa kaunti ya Lamu ni Bi Tashrifa Bakari (Ardhi na Mipangilio ya Mji), Bi Aisha Miraj (Utalii, Biashara na Utamaduni), Bi Sabrina Mkare (Uvuvi, Uchumi wa Bahari na Mifugo) na Bi Aisha Omar (Mabadiliko ya Tabianchi). Vilevile, kaunti hiyo ilijivunia mwaka uliopita wakati Bi Fahima Araphat Abdallah, mzaliwa wa Lamu, alipochaguliwa kuwa naibu mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).