BARAZA la Mitihani nchini (KNEC), limegundua kashfa katika baadhi ya shule za sekondari ambapo watahiniwa wao wa Mtihani wa Kitaifa wa Kidato cha nne (KCSE) walifanya mtihani wa Lugha ya Ishara (KSL) licha ya kutokuwa na ulemavu wa kusikia. KSL ni somo lililotengwa kutahiniwa kwa wanafunzi wa ulemavu wa kusikia. Hata hivyo wanafunzi wengine wana uhuru wa kusomea somo hilo bila ya kutahiniwa kwenye matokeo yao ya mtihani wa KCSE. Hata hivyo, katika mtihani wa mwaka jana, mamia ya wanafunzi wasiokuwa na ulemavu wa kusikia walijisajili kwa mtihani huo wa kitaifa. Matokeo yalipotangazwa na Waziri wa Elimu Bw Julius Ogamba wiki mbili zilizopita, walipigwa na butwaa walipogundua kwamba Knec haikujumuisha somo hilo ambalo walikuwa na matumaini lingeliwapiga jeki na kupata alama za kufuzu kujiunga na vyuo vikuu. Taifa Leo ilihoji baadhi ya watahiniwa ambao waliathirika na kashfa hiyo. Bi Winnie (sio jila lake kamili) alisema alianza kufanya somo hilo tangu Kidato cha Kwanza. Kijana huyo, 17 aliamini kuwa KSL ingekuwa tiketi yake ya kupata alama ya kujiunga na chuo kikuu moja kwa moja ili kusomea udaktari. Hata hivyo, matokeo yalipotolewa wiki mbili zilizopita, ndoto zake zilizimika. Somo la KSL, ambalo alilitegemea kusukuma wastani wa alama zake kutoka C- hadi C+, halikujumuishwa. Winnie ni miongoni mwa asilimia 84 ya watahiniwa wa KSL 3,493 waliofanya mtihani huo licha ya kutokuwa na ulemavu wowote wa kusikia. "Nililipenda sana somo hilo na sielewi ni kwa nini walimu wangu waliniacha niteseke kwa miaka minne kusomea somo ambalo walijua sitapata alama. Nilipata 'A' katika KSL lakini haikujumuishwa," alisema Winnie kwa uchungu. Watahiniwa wengi walikuwa wamechagua KSL ili kukwepa somo la Kiswahili. Badala yake, walijikuta na alama pungufu ambazo hawakuzitarajia. Wazazi wa Winnie walieleza kusikitishwa kwao baada ya kugundua kwamba KSL ni solo linalotumiwa kuwatahini wanafunzi wenye ulemavu wa kusikia pekee. "Kwa nini shule haikumwambia mtoto wangu mapema? Kwa nini mruhusu mtahiniwa asome somo kuanzia Kidato cha Kwanza hadi cha Nne?" aliuliza mzazi huyo. Knec ilishtumu walimu ambao waliruhusu wanafunzi hao kutahiniwa ilhali walijua kwamba haingelihesabiwa kwenye matokeo yao ya mitihani. Afisa Mkuu wa Knec Dkt David Njengere, alisema somo la KSL limehifadhiwa kwa ajili ya wanafunzi wenye ulemavu wa kusikia pekee. “Mtaala wa KSL uliandaliwa mahususi kwa wanafunzi wenye ulemavu wa kusikia na haujawahi kufanyiwa marekebisho kuhusisha wanafunzi wengine. Somo hilo lilianzishwa ili kupunguza changamoto za lugha wanazopata wanafunzi hawa katika Kiswahili, ambacho kinategemea sana matamshi ya sauti,” alisema Dkt Njengere. Knec iligundua udanganyifu huo kwa kufuatilia historia ya watahiniwa hao 3,493; wengi hawakuwa wamefanya KSL katika mtihani wa kitaifa wa darasa la nane (KCPE) na hawakuwa na rekodi za kuonyesha wana ulemavu wa kusikia. Mwenyekiti wa Chama cha Kitaifa cha Wazazi (NPA), Bw Silas Obuhatsa, alifichua kuwa visa vingi vimetoka katika shule za umma katika eneo la Kati. Alisisitiza kuwa walimu na walimu wakuu wanapaswa kuwajibika kwa kuwahadaa watahiniwa.