Mwanafunzi ashambuliwa na mbwa Iringa

Iringa. Rahimatullahi Ng’amilo (9), mwanafunzi wa darasa la nne katika Shule ya Msingi Nyumbatatu, Manispaa ya Iringa, ameshambuliwa na mbwa wazururaji wanne ambao wamemwachia majeraha katika sehemu mbalimbali za mwili wake. Tukio hilo limeibua upya hofu ya usalama wa watoto, changamoto ya udhibiti wa mbwa mkoani Iringa huku familia ya mtoto huyo ikilia na mzigo wa gharama za matibabu. Akizungumzia tukio hilo leo Januari 19, 2022 baada ya kuhojiwa na Mwananchi Digital Ofisa Mifugo wa Manispaa ya Iringa, Abishani Mwaisango, amekiri kuwepo kwa tatizo la mbwa wazururaji. Amesema hata walipomshambulia mtoto huyo msaada wa kutoa kibali cha matibabu ulitolewa haraka ili kuhakikisha anapata huduma za afya bila kuchelewa. Mwaisango amesema manispaa inaendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa kuwafungia mbwa wao kuanzia saa 11:00 alfajiri hadi saa 5:00 usiku ili kuzuia madhara kwa jamii, huku akisisitiza kuwa mbwa wanapaswa kufungwa kwa usahihi kwa kutumia minyororo au kuwekwa katika mabanda maalumu. Mwaisango ameeleza kuwa utoaji chanjo ya mbwa hufanyika kila baada ya mwaka katika kila kata, huku Manispaa ya Iringa ikikadiriwa kuwa na takribani mbwa 700, hata hivyo alidai kuwa changamoto ya utekelezaji wa kuwaua mbwa wazururaji kutokana na ushirikiano mdogo wa baadhi ya wananchi. Amesema awali mbwa wazururaji walidhibitiwa kwa kutumia bunduki, lakini kwa sasa mbinu mbadala ikiwemo matumizi ya mitego maalumu yenye chambo imeanza kutumika katika maeneo ya Manjinjio Ngelewala, Mwangata, Kitwiru, Mkimbizi, Kihesa, Mkwawa pamoja na dampo la Mwangata. "Jamii imekuwa haitoi ushirikiano wa kutosha kwa kutokuwafungia mbwa wao na kushindwa kubaini umiliki wa mbwa wanaozurura. Baadhi ya wananchi huwakataa mbwa wao wanapokuwa wazururaji, hali inayoongeza hatari kwa jamii," amesema Mwaisango. Amesema kuwa tatizo la mbwa wazururaji hujitokeza zaidi wakati wa msimu wa joto mwanzoni mwa kipindi cha mbwa kuzaana , ambapo mpaka sasa mbwa 29 wamepigwa risasi katika kata mbalimbali ikiwemo Mkwawa, Kwakilosa, Mkimbizi na Kihesa. “Hatua hii itaendelea kulingana na tathmini ya kitaalamu.” Kuhusu huduma ya kwanza kwa waathirika wa kung’atwa na mbwa, Mwaisango amesema hatua ya awali ni kuhakikisha mbwa anazuiwa ili asiendelee kuwashambulia watu wengine na vidonda vinapaswa kusafishwa kwa maji tiririka. Pia mwathirika anapaswa kupata huduma za matibabu mara moja ili kupunguza madhara na hatari ya maambukizi. Aliyemwokoa mtoto asimulia Mkazi wa eneo hilo, Kelvin Peter aliyemwokoa mtoto huyo, amesema mbwa waliomshambulia Rahimatullahi Ng'amilo walikuwa wanne na walikuwa wakali na kuwa alisikia kelele za mtoto akiomba msaada, hivyo kukimbia bila kusita kwenda eneo la tukio. “Nilipofika nilimkuta mtoto amezingirwa na mbwa wanne na alikuwa hana pa kukimbilia. Nililazimika kuwafukuza kwa kelele na nguvu ili kuokoa maisha yake," amesema Peter. Amesema tukio hilo limemuacha na hofu kubwa na kuwataka wananchi kuwajibika kwa kuwafungia mbwa wao ili kulinda usalama wa watoto na jamii kwa ujumla. Baba wa mtoto huyo, Said Ng’amilo, amesema alipokea taarifa za tukio hilo akiwa mbali na nyumbani. Ng'amilo ameiambia Mwananchi Digital kuwa alimkuta mtoto wake akiwa na majeraha makubwa na akilalamika maumivu makali na sasa anatibiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa ambako gharama za matibabu zimekuwa mzigo mkubwa kwake. Ng’amilo amesema mtoto wake amepelekwa kwenye chumba cha upasuaji mara mbili na pia amelazwa katika chumba cha uangalizi maalumu ambapo gharama za huduma hizo ni kubwa na zinaendelea kuongezeka kadri siku zinavyosonga. “Naendelea kupambana kadri ya uwezo wangu, lakini kinachonivunja moyo zaidi ni maumivu ambayo mtoto wangu hunieleza kila ninapomwona. Ni uchungu mkubwa kwa mzazi kumuona mtoto wake akiteseka” amesema Ng’amilo. Mwananchi Digital ilipofanya jitihada za kumtafuta Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa, Dk Alfred Mwakalebela kupitia ofisi ya Ofisa habari wa hospitali hiyo, ilielezwa kuwa iendelee kusubiri majibu kutoka kwa Mwakalebela, bila kuambiwa yatatolewa lini.