KIONGOZI wa Democracy for the Citizens Party (DCP), Bw Rigathi Gachagua, amempendekeza Mbunge wa Nyali, Bw Mohamed Ali, awe mgombea pekee wa ugavana Mombasa kupitia muungano wa upinzani. Bw Gachagua alisema mshirika mwenzake katika upinzani, ambaye ni Kiongozi wa Wiper, Bw Kalonzo Musyoka, amekubaliana na hayo lakini haijaamuliwa Bw Ali, almaarufu kama 'Jicho Pevu', atumie chama kipi. “Bw Musyoka ana umaarufu sana hapa Mombasa kama vile mimi na amekubali kumuunga mkono Bw Ali. Kile hatujaelewana ni chama gani atagombea kati ya Wiper na DCP. Lakini sisi ni kitu kimoja tutakubaliana,” alisema Bw Gachagua. Kulingana naye, mbunge huyo aliyechaguliwa kupitia UDA ameonyesha uongozi bora katika awamu zake mbili akiwa na rekodi ya maendeleo bila kashfa yoyote ya ufisadi. Wakati huo huo, Bw Gachagua alimtetea Bw Ali dhidi ya wanasiasa wanaomhusisha na ukabila, akisisitiza Mkenya yeyote ana haki ya kugombea ugavana Mombasa.