WAKILI Chris Kabiro anayeng’ang’ania umiliki wa jumba la Sh200milioni na Gavana wa Kirinyaga, Anne Waiguru amekata rufaa kupinga uamuzi wa mahakama kuu kutangaza hana haki kudai makazi hayo ya kifahari. Bw Kabiro aliwasilisha arifa katika mahakama ya rufaa kupinga uamuzi wa Jaji Oscar Angote kuamuru kwamba nyumba inayong’ang’aniwa ni ya Bi Waiguru. Jaji Angote alisema kwa mujibu wa ushahidi uliowasilishwa imethibitikaBi Waiguru ndiye mmiliki wa jumba hilo la kifahari. Aliamuru kampuni ya Kihingo Village (Waridi Gardens) Limited iliyomuuzia jumba hilo ikamilishe katika siku 30 mkataba wa mauzo ya jumba hilo. Pia Jaji huyo aliagiza kampuni ya Kihingo isimsumbue Bi Waiguru. Akitoa ushahidi kortini mmoja wa wakurugenzi wa Kihingo ambaye pia ni Mbunge wa Tetu James Ndung’u Gethenji alisema Bi Waiguru alinunua jumba hilo kwa bei ya Sh80milioni mnamo September 2015. Hata hivyo alisema gavana huyu hakukamilisha kulipia jumba hili kwa vile mzozo sugu ulizuka kati ya Bw Gethenji na ndugu zake. Baadhi ya wakurugenzi walishirikisha polisi kumtia nguvuni Ndung’u Gethenji na kumfungulia mashtaka na kupelekea mkataba wa mauzo ya jumba hilo kutifuka.