UNAPOMTEMBELEA mtoto wako shuleni au hata ukienda hospitalini, kabla ya kuruhusiwa kuingia ndani, mlinzi atakukaribisha na kitabu ambacho unafaa kuandika data zako za kibinafsi zikijumuisha jina, nambari ya kitambulisho na nambari yako ya simu. Baadhi ya shule, hospitali au hata majengo ya kazi hazijakumbatia teknolojia kuchukua data za wageni. Lakini swali tunalifaa kujiuliza ni je, kutumia kitabu ni salama? Hili ndilo swali ambalo limeibua mjadala baada ya baadhi ya wazazi katika mojawapo wa makundi ya WhatsApp kuanza kulalamika kuwa nambari zao za simu zilichukuliwa kutoka daftari la wageni shuleni na watu wasiojulikana. Kulingana na mzazi mmoja, alipokea ujumbe mfupi ukidai kuwa mwana wake anahitaji pesa za matumizi haraka. Ujumbe huo uliandikwa kana kwamba unatoka kwa mwalimu. Baadaye ilibainika kuwa kulikuwa na uwezekano wa maelezo yao kunakiliwa kutoka katika kitabu cha wageni. Kwa mujibu wa Robert Manyala, mkurugenzi wa kampuni ya Robiserch, huu ni mwanya mkubwa wa kiusalama ambao unaweza kuzibwa kwa kutumia zana za kidijitali za kusajili wageni. “Daftari la kawaida huruhusu kila mtu kuona jina, nambari ya simu na sababu ya ziara ya aliyekuja kabla yake. Hii ni hatari. Zana ya kidijitali huficha taarifa hizo na kuzihifadhi kwa usalama,” asema Manyala. Anasema mfumo wa kidijitali humwezesha mgeni kujaza taarifa zake kwenye kompyuta au simu, kisha taarifa hizo kuhifadhiwa kwa njia salama. Ni wahusika wachache tu wenye ruhusa wanaoweza kuzifikia. Katika shule, mfumo huo unaweza kusaidia kujua ni nani aliingia, saa gani na alimtembelea nani. Endapo kutazuka tatizo, uongozi unaweza kufuatilia kwa haraka bila kutegemea maandishi yasiyoeleweka au kurasa zilizochanika. “Teknolojia pia hutuma arafa kwa mhusika anayelengwa. Mwalimu au mwanafunzi anaweza kuthibitisha kuwa kweli ana mgeni kabla ya kumruhusu aingie,” aongeza. Manyala anasisitiza kuwa si shule pekee zinazopaswa kuzingatia mfumo huo. Ofisi za mashirika ya umma na binafsi pia ziko hatarini iwapo zitaendelea kutumia vitabu vya kawaida vya wageni. Katika baadhi ya matukio, watu wamekuwa wakitumia taarifa kuwalenga wafanyakazi kwa ulaghai au matangazo feki. Mfumo wa kidijitali hupunguza hatari hiyo kwa kuweka mipaka ya nani anaona nini. Aidha, mfumo huo hutoa takwimu muhimu kama idadi ya wageni kwa siku, saa zenye shughuli nyingi na hata historia ya ziara jambo linalosaidia kupanga usalama na huduma bora. “Usalama wa data ni sehemu ya usalama wa watoto na wafanyakazi. Taasisi zisiangalie gharama pekee, bali maadhara yanayoweza kutokea,” aonya Manyala. Katika dunia ambayo ulaghai wa mtandaoni unaongezeka, huenda wakati umefika wa kuaga daftari la wageni la karatasi na kukumbatia suluhu za kisasa zinazolinda taarifa na maisha ya watu.