ALIYEKUWA Naibu Rais Rigathi Gachagua amesema hawezi kushirikiana na Rais William Ruto kisiasa kwa kuwa hawana chochote kinachowaunganisha baada ya kufurushwa serikalini. Gachagua alisisitiza kuwa hawezi kufanya kazi na Rais Ruto katika mpango wa kisiasa wa baadaye. “Sidhani kama naweza kufanya kazi na UDA kwa sababu ajenda yetu kama Upinzani ni kumtoa Rais Ruto kutoka Ikulu kupitia kura katika uchaguzi ujao,” alisema Gachagua. Aliongeza; “Sisi ni wapinzani wake wakuu na hatuwezi kufanya kazi naye sasa kwani tunataka kuingia mamlakani na kufanya mabadiliko katika serikali kwa faida ya watu.” Alisema hana tofauti na jamii ya Wakalinji “kwa sababu ninashindana na Rais Ruto ambaye anakataa kusikiliza ushauri mzuri katika kuendesha serikali na kurekebisha uchumi.” Gachagua alisema licha ya wakazi wa Bonde la Ufa kumchagua kwa wingi katika Uchaguzi Mkuu wa 2022, eneo hilo halijafaidi kwa kiasi kikubwa kutokana na ahadi za maendeleo kutoka kwa utawala wa sasa. Alitaja miradi duni ya miundombinu ikiwemo barabara, maji na viwanja vya michezo kama baadhi ya ahadi ambazo utawala wa Kenya Kwanza umeshindwa kutekeleza. Gachagua aliwataka wakazi wa Bonde la Ufa kuchagua viongozi kutoka vyama tofauti badala ya kuweka tiketi zao zote kwa UDA pekee katika uchaguzi mkuu wa 2027. “Nawaambia wapiga kura wa Bonde la Ufa kuhakikisha hawaweki mayai yao kwenye kikapu kimoja katika uchaguzi ujao. Wapigie kura viongozi kutoka upande wa Rais Ruto na pia kutoka kwa upinzani kama njia ya kujihami,” alisema Gachagua. Gachagua alidai kuwa alitofautiana na Rais Ruto baada ya kumkosoa mara kadhaa kwa kushindwa kutekeleza ahadi za uchaguzi, kuacha mkakati wa uchumi wa awali na kudanganya Wakenya kuhusu masuala mbalimbali. “Nilitofautiana na Rais kwa kuwa alikosa kuthamini wale waliotuunga mkono katika Uchaguzi Mkuu wa 2022 na kubaki na wale waliotupinga. Ni kinyume cha maadili kuwatenga wale waliokuchagua,” alisema Gachagua. Akizungumza katika mahojiano ya moja kwa moja, Gachagua alieleza kuwa ana mpango wa kuondoa sifa ya kuwa kiongozi wa kabila la Mlima Kenya na kuzunguka nchi nzima kukutana na wapiga kura. Gachagua alisema atatembelea kaunti za Kisii, Nyamira, Narok, Nakuru, Bomet, Nandi na Kericho kwa lengo la kuuza chama chake cha DCP na kuzungumza na wakazi. Aliongeza kuwa hana mpango wa kushirikiana tena na Rais Ruto kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2027 baada ya mivutano iliyosababisha kuondolewa kwake madarakani Oktoba 2024. “Nitaenda kusikiliza watu wa Kenya, kama sehemu ya mchakato wa kushirikisha umma kuhusu mabadiliko wanayotaka kuona serikali ikifanya tutakapoingia mamlakani,” alisema Gachagua. Aidha, alisema kuwa DCP itafanya uteuzi wa haki na bila upendeleo katika uchaguzi wa 2027, akisema kuwa baadhi ya viongozi waliomwacha kwenye kona ya kisiasa Mlima Kenya walikuwa wanataka tiketi za moja kwa moja au walikuwa fuko wa Rais Ruto katika upinzani. Alisema kwamba uchumi utarekebishwa na kutakuwa na sera za kuhakikisha sekta ya kilimo ina faida ikiwa upinzani utachukua madaraka. Alizungumzia pia kuhusu elimu ya bure ya msingi na utekelezaji wa miradi ya miundombinu. “Biashara zinaanguka kutokana na ushuru mkubwa na mazingira duni ya kazi. Baadhi ya biashara zisizo rasmi zimebomolewa na serikali, na kuzuia watu kufanya biashara na kupata riziki,” aliongeza. Hata hivyo, alisema kuwa kodi ya nyumba nafuu, ambayo aliiunga mkono akiwa serikalini, itafutwa na michango irudishwe katika mishahara ya wafanyakazi.