MATUMIZI ya serikali kwa mpango wa ujenzi wa nyumba za bei nafuu yamezidi yale ya barabara kwa mara ya kwanza. Hii ni ishara ya mabadiliko ya kimkakati kuelekea miradi ya Rais William Ruto, huku ujenzi wa nyumba 200,000 za bei nafuu ukiendelea. Ripoti zinaonyesha kuwa Idara ya Serikali ya Makazi na Maendeleo ya Miji ilitumia Sh55.9 bilioni katika miezi sita hadi Disemba 2025, ikiwa ni ongezeko la Sh34.8 bilioni ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka 2024. Matumizi haya yamezidi matumizi ya fedha za ujenzi na ukarabati wa barabara kwa mara ya kwanza, huku Idara ya Barabara ikitumia Sh39 bilioni katika miezi sita, ikiwa ni upungufu wa Sh163 milioni ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka uliopita.