CHAMA cha United Democratic Alliance (UDA) kinachoongozwa na Rais William Ruto kitakabiliwa na mtihani mwingine mgumu kwenye chaguzi ndogo zitakazoandaliwa katika kaunti za Isiolo, Embu na Kakamega hapo Alhamisi Ijayo. Chaguzi hizo Februari 26 zitakutanisha serikali ya Kenya Kwanza na Muungano wa Upinzani katika kinyang’anyiro cha ubunge wa Isiolo Kusini, udiwani wa Evurore na Muminji eneobunge la Mbeere Kaskazini, na pia udiwani wa West Kabras katika eneobunge la Malava. Viti vya Evurore na Muminji katika Kaunti ya Embu viliachwa wazi baada ya wawakilishi wadi kujiuzulu kuwania ubunge wa Mbeere Kaskazini. Kiti cha Isiolo Kusini katika Kaunti ya Isiolo kilibaki wazi kufuatia kifo cha mbunge Mohamed Bidu. Kile cha West Kabras katika Kaunti ya Kakamega nacho kilibaki wazi baada ya Diwani David Ndakwa kuchaguliwa mbunge wa Malava. Mwaka jana, UDA ilishinda kwa kura chache katika uchaguzi mdogo wa Mbeere Kaskazini. Sasa upinzani unasema utakuwa macho kulinda kura zake ili kuzuia madai yoyote ya wizi. Katika eneo pana la Mlima Kenya, Rais Ruto anajaribu kurejesha umaarufu wake baada ya aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua kuondolewa madarakani. Ushindi kwa UDA utampa nafuu kisiasa chama hicho tawala kinapopania kuimarisha ushawishi wake mashinani. Kichapo kitapiga jeki pakubwa kambi ya Gachagua kuelekea uchaguzi mkuu 2027. Waziri wa Utumishi wa Umma Geoffrey Ruku na Gavana Cecily Mbarire wamekuwa mstari wa mbele kuwapigia debe wagombea wa UDA, wakisisitiza kuwa maendeleo ya barabara na maji yatategemea ushindi wa chama hicho. Katika Isiolo Kusini, siasa zimechukua sura ya ushindani wa kifamilia. Mgombea wa UDA Mohamed Tupi, mwenye umri wa miaka 36, anaungwa mkono na wazee wa Borana na viongozi wakuu wa eneo hilo. Hata hivyo, anakabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa dada yake Bina, binti wa pili wa marehemu mbunge, anayewania kwa tiketi ya Jubilee Party. Bina ameahidi kuchimba visima zaidi vya maji na kuboresha vile vilivyopo, pamoja na kushinikiza mpango wa lishe shuleni Wakati huo huo, mgombea wa National Economic Development Party (NEDP) Isaack Fayo alitangaza kujiondoa kumuunga mkono Tupi, hatua iliyozua mjadala mkali hasa baada ya kiongozi wa NEDP, Mike Sonko, kufanya kampeni kali na kutoa misaada mbalimbali kwa wakazi. Katika Wadi ya West Kabras, mgombea wa UDA Elphas Shalakha Kainanga anakabiliwa na ushindani mkali kutoka kwa Edward Indimuli wa Orange Democratic Movement (ODM) na wengine kutoka vyama tofauti. Wadi hiyo ina zaidi ya wapiga kura 11,000, na ushindani wake unaonekana kama kipimo cha ushawishi wa UDA dhidi ya upinzani katika Magharibi mwa Kenya. Kwa ujumla, chaguzi hizi ndogo ni jaribio muhimu kwa UDA na Rais Ruto katika juhudi za kuimarisha ngome zake kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2027. Matokeo yake yataonyesha iwapo chama tawala bado kina mizizi imara mashinani au iwapo upepo wa kisiasa umeanza kubadilika.