Mbunge adai uteuzi wa Oburu haukufuata sheria

CHAMA cha Orange Democratic Movement (ODM) kwa mara nyingine kimejikuta katikati ya mvutano wa uongozi, kufuatia madai kwamba uteuzi wa Seneta wa Siaya, Oburu Odinga, kuwa kinara wa chama haukufuata katiba ya chama. Hoja hii imeibuliwa na Mbunge wa Suba Kusini, Caroli Omondi, ambaye anadai mchakato mzima ulikuwa wa haraka na wenye dosari za kikatiba. Akizungumza katika mahojiano ya televisheni Jumatano, Februari 18, 2026, Omondi alisema katiba ya ODM iko wazi kwamba pindi nafasi ya uongozi inapokuwa wazi, mmoja wa manaibu wa kinara wa chama anapaswa kushika wadhifa huo kwa muda. Kwa mujibu wake, utaratibu huo haukufuatwa baada ya kifo cha aliyekuwa kinara wa chama, Raila Odinga. “ODM ilikuwa na manaibu wa kinara wa chama. Chini ya katiba ya chama, mmoja wao alipaswa kushikilia wadhifa huo kwa muda,” alisema Caroli, akisisitiza kwamba hivyo ndivyo inavyoelekeza katiba ya chama. Badala yake, anadai, Oburu Odinga ambaye wakati huo hakuwa na wadhifa rasmi wa juu ndani ya chama, “alipachikwa” kwenye uongozi bila kuzingatia taratibu. Mbunge huyo alidokeza pia uwezekano wa ushawishi wa nje, akisema maamuzi muhimu yalipitishwa kwa haraka chini ya maelekezo yasiyoeleweka, wakati baadhi ya viongozi wakuu wa chama walikuwa safarini India kurejesha mwili wa Raila Odinga nyumbani. Hata hivyo, uongozi wa ODM una msimamo tofauti. Kupitia taarifa rasmi, Baraza la Kitaifa la Uongozi (NGC) lilithibitisha uteuzi wa Oburu kama kinara wa chama, likisema hatua hiyo iliidhinishwa ipasavyo. Pamoja naye, Abdulswamad Sheriff Nassir, Godfrey Osotsi na Simba Arati walithibitishwa manaibu wa kinara wa chama. Uteuzi huo unatarajiwa kuidhinishwa rasmi na Mkutano wa Kitaifa wa Wajumbe (NDC). Wachaganuzi wa siasa wanasema kauli ya Omondi inazua maswali kuhusu demokrasia ya ndani ya chama. “ Je, kulikuwa na dharura iliyohalalisha kupuuza utaratibu wa kawaida? Au ni kweli kwamba katiba ya chama ilikiukwa kwa maslahi ya kisiasa?” anahoji mchaganuzi wa siasa Peter Opondo. Wafuasi wa Oburu wanasema uteuzi wake ulikuwa wa lazima ili kulinda uthabiti wa chama katika kipindi cha majonzi na mpito. Wanaeleza kuwa kama ndugu wa karibu wa Raila na mwanasiasa mkongwe, alikuwa chaguo la asili kuendeleza urithi wa kisiasa wa chama. Aidha, wanabainisha kuwa hatua hiyo ilipitishwa na vyombo halali vya chama. Lakini wakosoaji wanahoji kuwa hata katika mazingira ya dharura, katiba haipaswi kuwekwa kando. Kwao, kupuuza manaibu waliokuwapo kunazua maswali kuhusu heshima kwa taratibu na usawa wa ndani ya chama. Ikiwa chama kinachodai kutetea demokrasia hakiwezi kuheshimu katiba yake, kinawezaje kuhimiza utawala wa sheria kitaifa? Mvutano huu unajiri wakati ODM inajipanga kwa mustakabali bila kiongozi wake wa muda mrefu na ikikabiliwa na masuala nyeti kama ushirikiano wake na Rais William Ruto na maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa 2027. Uhalali wa uongozi wake, asema Opondo, ni jambo litakaloathiri mshikamano wa ndani na taswira ya chama kwa umma. “Swali la kama Oburu ni “kinara haramu” halitajibiwa kwa hisia bali kwa kurejea kwa katiba ya chama na maamuzi ya vikao halali. Ikiwa taratibu zilifuatwa, basi uongozi wake una msingi. Lakini ikiwa kulikuwa na mapungufu, basi ODM inapaswa kuyashughulikia kwa uwazi ili kurejesha imani ya wanachama wake,” asema. Katika kikao kilichoamua kuondolewa kwa Sifuna kama katibu mkuu wa ODM, Dkt Oburu alisisitiza kuwa yuko imara usukani mwa chama hicho. Mbunge wa Saboti, Caleb Amisi, pia amedai kuwa Oburu, anashikilia wadhifa wa kinara wa chama kinyume cha katiba ya chama. Akizungumza Jumamosi, Januari 24, 2026, Amisi alisema katiba ya ODM iko wazi kuhusu namna ya kumchagua kinara mpya pale nafasi inapokuwa wazi. Kwa mujibu wake, Kifungu cha 6-2-2 kinataka Mkutano Maalum wa Kitaifa wa Wajumbe (NDC) kuitishwa kumchagua si kumteua kinara mpya wa chama. “ODM imeundwa kwa misingi ya kikatiba. Ni ombwe gani la mamlaka? Je, mtu anaweza kuja tu na kujitangaza kinara wa chama? Hapana. Kwa nini? Kwa sababu tuna Kifungu cha 6-2-2 kinachosema Mkutano Maalum wa Kitaifa wa Wajumbe lazima uitishwe pale kinara wa chama anapofariki ili kuchagua, si kuteua, kinara mpya,” alisema Amisi. Mbunge huyo alisisitiza kuwa hadi sasa NDC hiyo haijaitishwa, jambo linalomfanya aamini kuwa Oburu yuko madarakani kinyume cha katiba ya chama. Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA), Winnie Odinga, pia amewahi kueleza mashaka, akisema hakukuwa na haja ya haraka kuteua kinara wa chama . Winnie alisisitiza kuwa miundo ya uongozi wa ODM kama Kamati Kuu ya Kitaifa (NEC) na Kamati Kuu Simamizi haziwezi kisheria kufanya maamuzi ya chama bila kupitishwa na NDC. “Katiba ya ODM inasema hakuna mwanachama wa Kamati Kuu au NEC anayeweza kutenda kwa niaba ya chama cha ODM isipokuwa waidhinishwe na NDC,” alisema, akiongeza kuwa baadhi ya wanaoshikilia nyadhifa kwa sasa “wanajiwakilisha isivyo halali” wakati ambapo chama kilipaswa kuwa kinatoa mwelekeo kwa wanachama. NEC ya ODM ambayo ilidai kumvua Sifuna wadhifa wa Katibu Mkuu imeitisha NDC Machi 27 mwaka huu.