Vigogo chipukizi kutoka Magharibi mwa Kenya

SIASA za Magharibi mwa Kenya zinaingia katika kipindi cha mpito ambapo vigogo wapya wanaibuka na kutishia ushawishi wa viongozi wa muda mrefu kama vile Musalia Mudavadi, Moses Wetangula, Eugene Wamalwa, na wengineo ambao wamekuwa wakitawala siasa za eneo hilo kwa muda mrefu. Miongoni mwa vigogo wapya wanaochipuka ni Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna, aliyekuwa Seneta wa Kakamega Cleophas Malala, Gavana wa Tranz Nzoia George Natembeya, na mbunge wa Saboti Caleb Amisi ambao wanaonekana kuunda kambi yenye nguvu inayojitahidi kupigania mabadiliko ya uongozi katika siasa za Magharibi. Bw Cleophas Malala ambaye alikuwa katibu mkuu wa UDA na sasa naibu kiongozi wa DCP, anajijengea umaarufu miongoni mwa vijana wa Magharibi na anachukuliwa kama mmoja wa wanasiasa wanaovutia wapigakura vijana. Gavana wa Trans Nzoia, George Natembeya, pia ni mmoja wa vigogo wapya wanaoibuka katika eneo hili. Natembeya, ambaye alitoka kwa utumishi wa umma katika sekta ya usalama, amejitokeza kama mpigania mabadiliko katika siasa za Magharibi kwa kuanzisha vuguvugu la "Tawe" ambalo limekuwa likipata ushawishi mkubwa katika sehemu ya vijana na makundi ya wananchi wanaotaka kuona mabadiliko makubwa katika uongozi wa Magharibi. Vuguvugu lake limepata ushawishi mkubwa na kutoa changamoto kwa vigogo wa zamani kama Mudavadi na Wetangula. Kwa upande mwingine, Caleb Amisi, Mbunge wa Saboti, anajiandaa kuwa sehemu muhimu ya upinzani kwa viongozi wa Magharibi. Amisi, ambaye ni mshirika wa karibu wa Sifuna, amejiweka katika mstari wa mbele katika siasa za Magharibi kwa kuonyesha nia ya kupigania haki za wananchi wa eneo hilo. Anapigania mabadiliko ya kisiasa na anataka kuona Magharibi ikitoka katika kivuli cha viongozi wa zamani na kujenga uongozi mpya wenye maono ya kisasa. Huku vigogo hawa wapya wakijitokeza, Musalia Mudavadi, Moses Wetangula, na Eugene Wamalwa, wakiwa na historia ndefu ya siasa katika Magharibi, wanajikuta katika hali ngumu. “Mudavadi, ambaye ni Mkuu wa Mawaziri katika serikali ya Rais Ruto, na Wetangula, ambaye ni Spika wa Bunge la Kitaifa, wamekuwa wakitajwa kama vigogo wa kisiasa katika Magharibi, lakini sasa wanakutana na changamoto kutoka kwa viongozi wapya wanaotaka kubadilisha mwelekeo wa siasa za eneo hilo,” asema mchanganuzi wa siasa Michael Wafula. Wachambuzi wanasema iwapo vigogo hawa wapya watapata umaarufu mkubwa na kushikilia wafuasi wao, basi wataweza kubadilisha mizani ya kisiasa katika Magharibi na kutishia nguvu za viongozi wa zamani. “Kwa sasa, siasa za Magharibi ziko katika kipindi cha mabadiliko, na kizazi kipya cha wanasiasa kimejiandaa kuchukua nafasi ya vigogo wa zamani. Muda utakuwa shahidi wa jinsi vigogo hawa wapya watakavyoweza kushinda au kushindwa katika vita vya kisiasa vya Magharibi,” asema Wafula.