Mezeni wembe, ninamuunga Sifuna, Ruth Odinga aapa

MWAKILISHI wa Wanawake Kaunti ya Kisumu, Ruth Odinga, kwa mara nyingine ameshikilia msimamo wake na kutangaza hadharani kumuunga mkono Katibu Mkuu wa ODM, Edwin Sifuna, anayekabiliwa na misukosuko ndani ya chama. Ruth, ambaye ni dada mdogo wa kiongozi wa ODM Oburu Odinga alisema alipinga na anaendelea kupinga juhudi za kumuondoa Sifuna katika wadhifa wake ndani ya chama. Bi Ruth alibainisha kuwa ingawa anaunga mkono misimamo na hatua nyingi za Sifuna, anatambua kuwa chama kwa ujumla kinaweza kuwa na mtazamo tofauti. “Namuunga mkono Edwin Sifuna katika mambo mengi anayofanya. Lakini kile ambacho chama kinahisi ni tofauti, mimi ni mmoja wa wale waliopinga kuondolewa kwa Sifuna,” alisema Ruth. Wiki mbili zilizopita, Sifuna alivuliwa wadhifa wa Katibu Mkuu wa ODM kufuatia kikao cha Kamati Kuu ya Kitaifa (NEC) kilichofanyika Mombasa, ingawa mahakama imesitisha uamuzi huo. Pia soma: https://taifaleo.nation.co.ke/siasa/binti-ya-mwanzilishi-wa-odm-winnie-odinga-akaidi-mjombake-aunga-mkono-sifuna/ ODM ilimteua Mwakilishi wa Wanawake wa Busia, Catherine Omanyo, kushikilia wadhifa huo kwa muda, huku kiongozi wa chama Oburu Odinga akiidhinisha uongozi wake. Mapema mwezi huu, Februari 2026, Ruth alimtetea Sifuna dhidi ya mashambulizi yaliyofuata mahojiano yake na kituo kimoja cha televisheni, ambapo alihoji chanzo cha fedha za mikutano mikubwa ya chama ya Linda Ground. Ruth pia alielezea wasiwasi wake kuhusu utekelezaji wa Makubaliano kati ya Rais William Ruto na marehemu kaka yake Raila Odinga, yaliyotiwa saini Machi 2025, akisema utekelezaji wake umekuwa wa kusuasua na kukosa nia ya kisiasa. “Katika miezi ya hivi karibuni, Seneta wa Nairobi na Katibu Mkuu wa ODM, Edwin Sifuna — pamoja na kundi la wanachama na wabunge wanaotajwa mara kwa mara kama ‘waasi’ — wamekuwa wakilaumiwa. Mvutano huu unatokana na Makubaliano kati ya Rais William Ruto na aliyekuwa Waziri Mkuu, Raila Odinga, iliyotiwa saini Machi 2025,” alisema Ruth. “Lakini ni mashambulizi yaliyofuata mahojiano yake ya hivi karibuni kwenye Citizen TV yaliyonifanya nijiulize jinsi misimamo ya kisiasa hubadilika kwa haraka. Anauliza maswali yale yale ambayo tumekuwa tukiuliza licha ya mashambulizi ya mtandaoni kutoka kwa wanablogu walioajiriwa?” Ruth alihoji.