Mamba watundu waendelea kuangamiza wakazi

KWA miongo mingi, fuo za Ziwa Turkana zilikuwa zikikidhi maisha ya wavuvi. Lakini miaka ya hivi karibuni, maji yametishia maisha yao. Mamba ambao wameongezeka kwa sababu ya kujaa kwa maji na kuvurugwa kwa makazi yao asili, sasa wanatembea karibu na makazi ya watu. Mashambulizi yameongezeka, yakisababisha vifo vya angalau watu watatu kila mwezi, na kuacha wengi na majeraha na kulazimisha mbinu za jadi za uvuvi kuwa hatarini kutoweka. “Kwa sasa, hatuwezi kusema ni sehemu gani ya ziwa iko salama. Maji yamejaa na kuzingira maeneo yetu ya jadi ya uvuvi. Sijawahi kuona kitu kama hiki katika miaka yangu yote,” anasema mvuvi Joseph Mutei kwa sauti yenye machungu. Kwa jamii zinazozunguka Ziwa Turkana, mamba si tu wanyama wanaohatarisha maisha, bali ni tishio la moja kwa moja kwa ustawi wao. Pia soma: https://taifaleo.nation.co.ke/makala/huyu-hapa-padri-anayefuga-mamba-kobe-na-nyani-nandi/ Hata juhudi za hivi karibuni za Shirika la Huduma za Wanyamapori Kenya (KWS) hazijafanikiwa kurekebisha hali. Mnamo Januari 15, 2026 maafisa wa KWS waliua mamba mkubwa aliyezua hofu katika kijiji cha Kakwanyang, lakini mashambulizi yaliongezeka sehemu nyingine za ziwa. James Ekutan, mvuvi katika kijiji cha Namukuse, anasema, “Tunaishi huku tukitishiwa kila wakati. Kati ya Julai na Agosti 2025, jamii yetu iliandikisha mashambulizi manne. Mengi hayaripotiwi kutokana na mitandao mibaya ya mawasiliano.” Pia soma: https://taifaleo.nation.co.ke/makala/kitui-makueni-zachukua-hatua-kudhibiti-hatari-ya-mambaviboko/ Gavana wa Turkana, Jeremiah Lomorukai, anakadiria kuwa zaidi ya watu 40 wameuawa na mamba karibu na ziwa. Katika ziara yake ya hivi karibuni eneo la Kerio Delta, alikutana na familia zilizopoteza wapendwa na riziki zao. Ili kupambana na tishio hilo, alitangaza kuwa atapatia wavuvi wa Kerio, Kalokol na maeneo mengine mashua za uvuvi, kama sehemu ya mpango wa kudhibiti kero ya mamba.