WATU watatu walifariki papo hapo na kadhaa kujeruhiwa baada ya magari waliyokuwa wakisafiria kuhusika katika ajali kwenye barabara ya Nairobi-Mombasa. Ajali hiyo ilitokea saa nane na nusu alasiri katika Mlima Kiu karibu na Kituo cha Mafuta cha Rubis, wakati dereva wa lori aina ya Mercedes Benz Actros alipojaribu kupita magari mengine kadhaa na kugongana na magari matano. Kamanda wa Polisi wa Mukaa, Abduba Hussein, alithibitisha ajali hiyo. “Ilitokea wakati dereva asiyejulikana, ambaye alikimbia baada ya ajali, alikuwa akielekea Mombasa kutoka Nairobi. Alipofika kwenye eneo hilo, bila tahadhari, alijaribu kupita magari mengi, na kugonga magari matano,” Hussein alisema. Hussein alisema kuwa ajali ilitokea kwenye mteremko mkali wakati wa mvua, na akawataka madereva kuzingatia sheria za barabarani ili kuepuka kupoteza maisha. Katika kisa tofauti siku hiyo hiyo, mtembea kwa miguu alifariki baada ya kugongwa na gari lililotoroka katika eneo la Kautandini kwenye barabara hiyo. Hussein alithibitisha kuwa mwili wa mtembea kwa miguu huyo alipelekwa katika mochari ya hospitali ya Kaunti ndogo ya Kilungu.