GHARAMA ya ujenzi wa Talanta Sports City Jijini Nairobi imeongezeka kwa Sh10.85 bilioni, Mkaguzi Mkuu wa Hesabu, Nancy Gathungu, amefichua. Katika ripoti mpya, Bi Gathungu anahoji mabadiliko ya bei yasiyojulikana kwa ujenzi wa uwanja huo wa michezo wa viti 60,000 Jijini Nairobi, akisema kuwa utoaji wa zabuni ulikiuka sheria za ununuzi na hakukuwa na idhini ya Mwanasheria Mkuu. Ukaguzi unaonyesha kuwa Wizara ya Fedha ilikubali ufadhili wa mradi wa Sh35 bilioni, kupitia Hazina ya Maendeleo ya Michezo na Sanaa (SASDF). “Hii ni kinyume na kiasi cha mkataba cha Sh45.85 bilioni, ongezeko la Sh10.85 bilioni,” ripoti ya ukaguzi inaonyesha. Ufichuzi wa Dkt Gathungu katika ripoti ya ukaguzi wa Wizara ya Ulinzi kwa kipindi cha fedha cha 2024/25 iliyowasilishwa bungeni, unamuweka Katibu wa Ulinzi, Patrick Mariru, katika hali tata. Mkaguzi Mkuu pia anaonya kwamba kuchelewa kulipa mkandarasi kutazaa riba ya asilimia tatu juu ya kiwango cha wastani cha riba cha Benki Kuu ya Kenya (CBK) kwa mikopo, na hivyo kuongeza gharama ya mradi. Mbali na gharama kuongezeka kwa kile kinachosemekana kuwa ni uwanja mkubwa na wa kisasa wa soka nchini Kenya, ukaguzi unaeleza wasiwasi kwamba kibali hakikupatikana kutoka kwa Mwanasheria Mkuu kabla ya kutoa mkataba. Zaidi ya hayo, ukaguzi unazua wasiwasi kuhusu ukweli wa kifedha wa mradi, kwani unaonyesha kuwa maelezo ya ufadhili hayakutolewa kwa wakaguzi, na Bi Gathungu anasema kuwa ukaguzi maalum pekee ndio utatoa majibu kuhusu thamani ya fedha katika utekelezaji wa mradi huo. Ongezeko la Sh11 bilioni zilizofichuliwa katika mradi huo zinatosha kujenga kilomita 9.5 za barabara ya Rironi-Mau Summit kwa gharama ya Sh1.14 bilioni kwa kila kilomita. Pia soma: https://taifaleo.nation.co.ke/michezo/rais-ruto-afurahishwa-na-ujenzi-wa-uwanja-wa-talanta/ Gharama iliyoongezwa katika mradi huo pia inatosha kugharamia wanafunzi milioni 4.8 katika shule za msingi au wanafunzi 487,000 wa shule za sekondari kwa mwaka mzima kulingana na viwango vya sasa vya serikali vya udhamini wa wanafunzi. Inagharimu serikali Sh2,238 kwa mwaka kugharamia elimu ya mwanafunzi katika shule ya msingi ya umma na Sh22,244 kumfundisha mwanafunzi katika shule ya sekondari za umma kwa mwaka. Katika visa vya hivi karibuni, kama alivyothibitisha Waziri wa Fedha John Mbadi, serikali imeweza kutoa takribani Sh16,900 kwa kila mwanafunzi wa shule ya sekondari, ambayo ina maana kuwa Sh10.85 bilioni zinaweza kugharamia ufadhili wa wanafunzi 642,000. Ikiwa fedha zingetumika kwa wanafunzi wa Shule ya Sekondari Msingi (JSS), angalau wanafunzi 721,000 wangeweza kufadhiliwa kwa kiwango cha Sh15,042 kwa kila mwanafunzi. Ripoti ya ukaguzi ilijiri huku Mbunge wa Kiharu, Ndindi Nyoro, akidai kwamba gharama ya uwanja wa soka wa Talanta itakapomalizika kulipwa, taifa litakuwa limelipa zaidi ya Sh100 bilioni. Bw Nyoro aliongoza Kamati ya Bajeti na Ugavi ya Bunge la Kitaifa kabla ya kutimuliwa alipotofautiana kisiasa na Rais William Ruto. Ukaguzi unaonyesha kuwa Wizara ya Ulinzi ilitia saini mkataba wa miaka miwili na mkandarasi wa kigeni Mei 26, 2024, kubuni na kujenga Talanta Sports City kwa Sh45.85 bilioni. Ripoti inaonyesha kwamba “kibali kutoka kwa Mwanasheria Mkuu hakikutolewa kwa wakaguzi.” Wakati huo, BwJustin Muturi alikuwa Mwanasheria Mkuu. Sehemu ya 134 ya Sheria ya ununuzi wa Umma inasema kuwa afisa mkuu wa hesabu wa taasisi ya ununuzi atahakikisha kuwa mikataba yote ya thamani ya zaidi ya Sh5 bilioni inapata kibali kutoka kwa Mwanasheria Mkuu kabla ya kutiwa saini.