Makundi 3 yapata pigo kwenye kesi ya kutetea mashoga

MAHAKAMA Kuu ya Mombasa imezuia mashirika matatu yanayotetea haki za jamii ya wapenzi wa jinsia moja (LGBTQ) nchini kujiunga na kesi ya kupinga madai ya uchochezi wa vurugu unaolenga watu wanaojitambulisha kama wanachama wa jamii hiyo. Mahakama ilibainisha kuwa, ombi hilo halikuwasilishwa na mlalamishi katika kesi hiyo bali na mtu ambaye, kwa madhumuni yote, ni mgeni katika suala lililo mbele ya mahakama. Katika uamuzi uliotolewa Februari 20, mahakama ilieleza kuwa, ingawa mlalamishi angeweza kuomba kuingiza mhusika mwingine katika kesi, hakuna kilichowazuia pia wahusika waliopendekezwa kuchukua hatua na kuwasilisha maombi yao ipasavyo mahakamani. Mahakama ilisema hakuna mwakilishi yeyote wa waliotakiwa kuingizwa kama mlalamishi wala wahusika waliowasilisha ombi hilo. “Kwa msingi huo, ombi hilo halifai na lina dosari kubwa. Kwa sababu hii, ombi limekataliwa,” mahakama ilisema. Katika kesi hiyo, wanaharakati wanaopinga LGBTQ pamoja na Mbunge wa Nyali Mohamed Ali wameshtakiwa kwa madai ya kuchochea wananchi kutekeleza mauaji ya kiholela au kudhuru watu wanaojitambulisha kama wanachama wa jamii hiyo. Mwaka 2024, Mahakama Kuu ya Mombasa ilitoa amri za muda kuzuia uchochezi dhidi ya jamii ya LGBTQ na pia kuzuia wanaharakati wanaopinga jamii hiyo kuhimiza kufukuzwa kwa watu wanaojitambulisha kama LGBTQ kutoka nchini au kufungwa kwa mashirika yanayohudumia jamii hiyo. Mnamo Septemba 2024, ombi liliwasilishwa likitaka mashirika matatu yaunganishwe katika kesi hiyo kama mlalamishi mwenza na kama wahusika wenye maslahi. Pia soma: https://taifaleo.nation.co.ke/habari/habari-za-kitaifa/wabunge-waonywa-dhidi-ya-kupitisha-mswada-unaoharamisha-lgbtq/ Mashirika hayo ni pamoja na Generation of Holistic Partners Network (GHPN), Gay and Lesbian Coalition of Kenya na Kenya Legal and Ethical Issues Network on HIV and AIDS (KELIN). Ombi hilo linaungwa mkono na hati ya kiapo iliyoapwa na Bw Ishmael Omumbwa Ondunyi, anayejitambulisha kama mwenyekiti mwenza wa GHPN na Mkurugenzi Mtendaji wa PEMA Kenya, mwanachama wa chama kingine kilichopendekezwa kuingizwa kama mhusika wa nne mwenye maslahi. Katika hati yake ya kiapo, Bw Ondunyi pia anadai kuwa tangu Machi 2023, washtakiwa waliandaa kile walichokiita “maandamano ya kupinga LGBTIQ+” kote nchini, yakidaiwa kuchochea vurugu dhidi ya wanachama wa jamii hiyo na mashirika yao. Aidha, anadai kuwa kutokana na hilo, baadhi ya mashirika yalilazimika kufungwa. Anataja matukio ambapo Kliniki ya Mvita na za HAPA Kenya huko Mombasa na Voi zilivamiwa na kufungwa kwa nguvu, jambo lililokatiza upatikanaji wa huduma za afya. Kulingana na hati hiyo, muungano huo unakusudia kuonyesha jinsi vitendo vinavyodaiwa vya kupinga LGBTIQ+ vilivyoathiri moja kwa moja utu, maisha ya kila siku na haki za kimsingi za watu waliotengwa, na kuongeza hatari za kiafya, changamoto za afya ya akili na kutengwa kijamii. Hata hivyo, Bw Salim na Bw Ahmed, ambao ni washtakiwa katika kesi hiyo, walipinga ombi hilo wakisema hakuna ushahidi kwamba mwapaji wa hati ya kiapo iliyowasilishwa kuunga mkono ombi hilo alikuwa ameidhinishwa ipasavyo kuapa kwa niaba ya mlalamishi aliyependekezwa. Kulingana nao, maandamano yanayotajwa yalikuwa ya amani bila uchochezi wa vurugu wa aina yoyote na waandamanaji walikuwa wakitekeleza haki zao za kikatiba kwa njia halali.