MUUNGANO mpya wa kisiasa unaibuka nchini kwa kasi huku ukitishia kuvuruga hesabu za kisiasa katika uchaguzi wa 2027. Huu, kimsingi, si muungano wa upinzani bali ni kundi la wabunge vijana wanaopambana kujiondoa katika kivuli cha vyama vyao vya kisiasa kwa lengo la kufanya vigumu Rais William Ruto kushinda muhula wa pili. Kufikia mwaka jana, Februari 22, 2026 uchaguzi wa 2027 ulionekana kuwa ushindani kati ya Rais Ruto na mgombeaji wa upinzani. Hata hivyo, Linda Mwananchi, inayomaanisha 'linda raia', ikiongozwa na Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna, inatishia kuvuruga mpangilio wa tangu jadi wa 'farasi wawili' wakati wa uchaguzi kwa kujitambulisha kama 'sauti mbadala'. Vuguvugu hili linazidi kugeuka kuwa nguvu kubwa ya kisiasa itakayokuwa vigumu kupuuza; likijiandaa kuwa mrengo wa nguvu tatu kuelekea uchaguzi mkuu ujao. Mbinu zao za kuvutia umati na kupigania ukweli dhidi ya utawala, tayari zinazua mawimbi ya kisiasa kote nchini, na kutatiza mirengo iliyokuwepo hapo awali. Wakiungwa mkono na umati katika mikutano yao ya Kitengela na Kamamega, viongozi wa vuguvugu hili sasa wanajitahidi kuvuruga mirengo ya kawaida katika uchaguzi wa Kenya. Pia soma: https://taifaleo.nation.co.ke/habari/mezeni-wembe-ninamuunga-sifuna-ruth-odinga-aapa/ Kundi hili limechochewa na maamuzi ya hivi karibuni yaliyofanywa na Chama cha ODM kumfukuza katibu mkuu wake, Seneta Sifuna na pia kuanza rasmi mazungumzo na Chama cha UDA cha Rais William Ruto. Maamuzi hayo yalichafua mazingira ya kisiasa nchini. Mbali na Seneta Sifuna, wanachama wengine maarufu katika kundi hili ni Mbunge wa Embakasi Mashariki, Babu Owino, Seneta wa Vihiga Godfrey Osotsi, Gavana wa Siaya James Orengo, Mbunge wa Saboti Caleb Amisi, na binti wa marehemu Raila Odinga, Winnie Odinga. Viongozi hawa, wengi wakitoka ODM, wamekuwa wakikosoa kwa nguvu mpango wa Serikali Jumuishi. Wameanza pia kupima hali ya kisiasa kwa uwezekano wa kutoa mgombea urais. “Tunataka kumwambia Sifuna aendee urais,” alisema Mbunge wa Kabuchai, Majimbo Kalasinga mnamo Jumamosi uwanjani Amalemba, Kakamega. Viongozi wa kundi hili hawana mizigo ya kisiasa ukilinganisha na Rais Ruto au viongozi wengine wa upinzani kama Rigathi Gachagua wa chama cha DCP, Kalonzo Musyoka wa Wiper na Fred Matiang’i wa Jubilee. Akizungumza na Taifa Leo jana, Jumapili, Februari 22, Bw Amisi alisema kuwa wao si farasi wa tatu bali ndio farasi wa pekee. Pia soma: https://taifaleo.nation.co.ke/siasa/wanachama-wa-uda-wakasirishwa-na-sifuna-kwa-kuyumbisha-odm/ Aidha, alisema wanapata nguvu kutoka kwa vijana. “Vijana wamechoka na wako tayari kubadilisha uongozi nchini. Unaweza kuona jinsi tunavyovutia umati mkubwa. Hasira hiyo inatokana na viongozi wanaoendelea kuiba pesa zao na kuonyesha maisha ya anasa, na matumizi mabaya ya fedha,” alisema Bw Amisi. “Sisi si farasi wa tatu bali ni farasi wa pekee. Sisi sio waasi bali tunafanya kazi kwa msingi wa demokrasia,'” akasema Babu Owino. Ingawa kundi hili limewahi kuashiria ushirikiano na viongozi wa upinzani ili kuunda muungano wa kisiasa kupambana na Rais Ruto, liko tayari pia kujisimamia. “Tumesema kuwa bila kujali hali itakavyokuwa, tutaendelea kuwa pamoja. Tuko tayari kujiweka hatarini kwa ajenda tunayoamini. Hatutakaa kimya tukiangalia mambo mabaya yanayotokea nchini kwetu,” aliongeza Bw Owino. Mtaalamu wa masuala ya kisiasa, Macharia Munene anasema kuwa kundi la Linda Mwananchi linatikisa nchi kwa sababu watu wanaamini lina viongozi wanaoweza kutekeleza masuala yao, jambo ambalo pande nyingine mbili zimeshindwa kudhihirisha. Alisema mkutano wa Kitengela ulikuwa hatua muhimu kwao na mkutano wa Kakamega ulithibitisha mafanikio ambayo kundi hili limepata.