NAIBU Rais Kithure Kindiki ametoa wito wa kampeni za amani kuelekea kwa uchaguzi mdogo wa udiwani utakaofanyika Februari 26, 2026. Akizungumza katika kanisa la Kanthoki Full Gospel katika eneobunge la Mbeere Kaskazini, Kaunti ya Embu huku akipigia debe mwaniaji wa UDA Duncan Muratia wa kiti cha Evurore, Prof Kindiki alitaka makundi pinzani kudumisha amani. “Ushindani wa kisiasa si uadui, tufanye kampeni bila ghasia,” alisema. Alieleza imani yake kwamba UDA itashinda viti vyote katika uchaguzi huo akitaja kampeni kali inayoendeshwa na vigogo wa serikali, Waziri Geoffrey Ruku na Gavana wa Embu Cecily Mbarire. Katika wadi ya Muminji, mfuasi wa chama cha Devolution Empowerment Party alidungwa kisu na kufariki wakati wa kampeni. Kijana huyo, Benard Kithaka, 24, alidungwa kisu Februari 18 baada ya kudaiwa kukataa kuvalia kofia ya UDA. Kulingana na kiongozi wa DEP Lenny Kivuti, wafuasi wa UDA walimkabili Kithaka na kujaribu kumlazimisha kuvalia kofia ya chama tawala lakini akakataa. Hapo ndipo mmoja wa wafuasi wa UDA alichomoa kisu na kumdunga Kithaka tumboni, na kumwacha akigaragara chini kwa uchungu mwingi. Alikimbizwa katika hospitali moja ya kibinafsi ila akatangazwa kuwa amefariki. Bw Kivuti alisema ilikuwa huzuni kubwa kwamba kijana Kithaka alipoteza maisha yake kwa sababu ya siasa mbaya. “Kithaka, mwanachama wa DEP kutoka Ndutori, Muminji alidungwa kisu na kufariki na mfuasi wa UDA kwa sababu ya kitu kidogo tu kama kuvalia kofia ya UDA ambayo alikataa,” akasema Bw Kivuti. Alikemea vikali tukio hilo na kutaka polisi kufanya uchunguzi upesi na kuhakikisha wahusika wamekamatwa na kufunguliwa mashtaka.