Kusimamishwa kazi kwa mkuu wa hospitali kwaanika mahangaiko ya kimya kimya ya wagonjwa

HATUA ya Serikali ya Kaunti ya Mombasa kumsimamisha kazi kwa muda Afisa Mkuu wa Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Coast General, Dkt Iqbal Khandwalla, imeanika wazi changamoto ambazo zimekuwa zikitatiza hospitali hiyo kimyakimya kwa muda mrefu. Hospitali hiyo iliyo maarufu kama Makadara, ambayo hutegemewa na maelfu ya wakazi hasa wenye kipato cha chini kutoka kaunti zote sita za Pwani, imekuwa ikilalamikiwa kwa kudorora kwa huduma za afya kwa karibu miaka mitatu sasa. Wakati wa kuanzishwa kwa serikali za ugatuzi zaidi ya miaka 10 iliyopita, hospitali hiyo ilikuwa fahari ya Pwani kwa kuanzisha upasuaji wa moyo na mbinu za kisasa za matibabu. Hii leo, wagonjwa wengi wanaeleza changamoto walizokumbana nazo wakisaka matibabu na hata familia zengine kudai wapendwa wao walifariki kutokana na utepetevu, huku wahudumu wa afya wakisema hawapewi rasilimali za kutosha kutekeleza majukumu yao. Licha ya changamoto hizi, viongozi wengi wa Mombasa walikuwa wamesalia kimya hadi wikendi, wakati mfanyakazi wa afisi ya eneobunge la Mvita alipofariki hapo. Ali Kibwana, 52, alianguka na kupata jeraha kichwani ndipo akakimbizwa hadi katika hospitali moja ya kibinafsi kabla ya kupewa rufaa hadi Coast General. Hata hivyo familia ya mgonjwa huyo ilidai kuwa, msimamizi wa hospitali hiyo, Dkt Khandwalla alikataa kumpeleka katika chumba cha wagonjwa mahututi hadi pale watakapolipa ada yote iliyotakikana. “Tulilipa zaidi ya Sh100,000 tukaambiwa lazima tulipe ada yote kabla aingizwe kwenye chumba cha wagonjwa mahututi. Hakutibiwa kwa wakati, akaaga dunia. Kama wanaweza kufanyia mtu kama sisi ambao tuna uwezo, je maskini?” familia hiyo iliuliza. Mbunge wa Mvita, Bw Masoud Machele, naye akampa makataa Gavana Abdulswamad Nassir kumchukulia hatua kali Dkt Khandwalla kwa madai ya utepetevu. Alidai kuwa, bila kufanya hivyo, gavana atakosa kura za wakazi wa Mombasa. “Gavana ni ama utasimama na sisi wananchi au Dkt Khandwalla kwa sababu hatuwezi kuendelea kupoteza wapendwa wetu kila kuchao sababu ya utepetevu katika hospitali hii,” alisema Bw Machele. Baadaye Jumapili, Afisi ya Katibu wa Kaunti ilitoa taarifa kutangaza kuwa, Bodi ya hospitali hiyo ilikutana na kuamua kumsimamisha kazi kwa muda Dkt Khandawala ili kutoa nafasi ya kutatua masuala yaliyoibuka kuhusu utendakazi duni. Dr Sood Mohamed alipewa wajibu wa kushikilia nafasi hiyo hadi wakati mwelekeo mwingine utatangazwa. Hata hivyo, Dkt Khandwalla alipinga madai hayo akisema hata kabla ya kupigiwa simu na Mbunge huyo madaktari walikuwa wameanzisha juhudi za kuokoa maisha ya mgonjwa ambaye alifikishwa akiwa hali mbaya. “Mbunge alinipigia simu akitaka nimsaidie mgonjwa wake na tulimsaidia. Tulifanya ukaguzi wa kiafya maarufu kama MRI na tukagundua alikuwa anavuja damu," akasema, akiongeza kuwa mgonjwa huyo alikuwa chini ya mtaalamu wa upasuaji wa ubongo, Dkt Ben Okanga. Dkt Khandwalla alisema hakupinga mgonjwa huyo kupelekwa ICU kama alivyodai mbunge huyo. “Huo ni uongo, mimi si daktari wa upasuaji wa ubongo,” alisema Dkt Khandwalla. Dkt Okanga naye alifafanua matukio ya siku hiyo, akisema mgonjwa alifikishwa akiwa amevuja damu sana. “Tulifanya juhudi zote lakini hatukufaulu kwa sababu alikuwa amevuja damu sana. Wagonjwa wengi wanaoletwa wakiwa hali hiyo huwa hawamalizi siku 30 huku wengine wakiaga dunia papo hapo,” alisema Dkt Okanga. Alisema mgonjwa hangefanyiwa upasuaji kwa sababu hali yake ilikuwa imedhohofika. Hata hivyo alipelekwa ICU kama inavyotakikana chini ya kanuni za kimatibabu. “Si eti aliaga dunia kwa sababu tulikataa kumtibu, hapana. Alikuwa mgonjwa sana na katika hali yake hangeweza kufanyiwa upasuaji,” alisema Dkt Okanga. Kufuatia kisa hicho, serikali ya kaunti ilimsimamisha kazi kwa muda Dkt Khandwalla, hali iliyoanika peupe masuala mengine ambayo pengine hayakukusudiwa. Chama cha Madaktari nchini (KMPDU) kilikosoa serikali ya kaunti kwa kumsimamisha kazi Dkt Khandwalla wakisema si haki. Viongozi wa chama hicho walitoa ilani ya siku saba kwa serikali ya kaunti kumrudisha kazini la sivyo waanze mgomo. Mwenyekiti wa chama hicho, Dkt Abidan Mwachi, alisema Mbunge alishinikiza matibabu ya haraka kwa sababu mgonjwa alikuwa mfanyakazi wake, jambo ambalo ni kinyume na miongozo ya kitabibu. Chama hicho sasa kinafikiria kuchukua hatua za kisheria dhidi ya Mbunge huyo kwa kukiuka maadili ya uongozi. Dkt Khandwalla aliajiriwa na aliyekuwa Gavana Hassan Joho karibu mwongo mmoja uliopita na alipewa mamlaka kamili ya usimamizi. Hatua hiyo ya utawala wa Joho uliwezesha hospitali kupata ufadhili mkubwa wa wafadhili, hali iliyoboresha pakubwa mazingira ya utendakazi na utoaji huduma. Mbunge Mwakilishi wa Kike wa Kaunti ya Mombasa, Bi Zamzam Mohammed, alimkosoa Gavana Nassir akisema uamuzi wake unahujumu uongozi wa hospitali. “Dkt Khandwalla alileta maendeleo katika hospitali hii ya umma. Kwa nini alifaulu wakati wa Gavana Joho lakini sasa anashindwa? Ukweli ni kwamba uongozi wa sasa unaingilia usimamizi wa hospitali," akasema. Kulingana naye, ripoti zimeonyesha kuwa hospitali hiyo inadai Hazina ya Afya ya Umma (SHA) mamilioni ya pesa na inashindwa kuendeleza majukumu yake ipasavyo. Wahudumu wa afya walioomba kutotajwa kwa kuhofia kuadhibiwa, walithibitisha kuwa, mara nyingi wao hutatizika kupata hata mahitaji madogo yanayotakikana kuhudumua wananchi. Seneta wa Mombasa, Bw Mohamed Faki, alisema serikali ya kaunti inamsukumia daktari huyo lawama badala ya kutatua changamoto halisi zilizomo. Alisema kuwa, kwa miaka mitatu, serikali ya kaunti imekuwa ikilipa mishahara pekee bila kuwekeza kwenye miundomsingi. Baadhi ya masuala hayo yaliangaziwa na kamati ya seneti iliyotaka uwajibikaji hivi majuzi. Kamati ya Afya ya Bunge la Kaunti ya Mombasa imeandikia barua bodi ya CGTRH ikitaka majibu kuhusu masuala yaliyoibuka. Seneta Maalumu, Bi Miraj Abdillah, ametoa wito wa ukaguzi wa kina kuhusu idadi ya wafanyakazi na viwango vya malipo ya hospitali hiyo.