FAMILIA ya mlinzi wa Muungano wa Wahudumu wa Bodaboda Kisumu inasaka haki kuhusu mauti yaliyotokea Mbale kutokana na makabiliano kati ya wafuasi wa Linda Wananchi na wale wanaorindima ngoma ya 'Tutam’. George Olwande Otobe inadaiwa alikuwa atoe ulinzi kwa wanasiasa wa Linda Mwananchi katika mkutano wao mjini Kakamega na Vihiga. Hii ni kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Muungano wa Wahudumu wa Bodaboda Kisumu Jacob Ogamba. “Alikuwa mkuu wa usalama wetu na tunasaka haki kwa familia yake na wahudumu wote wa bodaboda,” akasema Bw Ogambo. “Alikuwa akiunga viongozi wa Linda Mwananchi na alipofika Mbale, aliandamwa na kundi mmoja waliomtambua na kumvamia. Tunaamini Olwande alifuatwa na wahuni baada ya kuondoka Kisumu,” akaongeza. Mkewe Florence Atieno naye amesimulia kwa masikitiko jinsi alivyofahamishwa kuhusu mauti ya mumewe ambaye walikuwa wameagana asubuhi na hata akamwaachia hela za matumizi. “Niliona picha yake akiwa amelowa damu na ikaandikwa amefariki kisha nikapigiwa simu na mwanamke kutoka Mbale aliyeniambia mwili wake umepelekwa katika mochari. Nilisikitika na siwezi kukumbuka kilichotokea baada ya hapo,” akasema Bi Atieno. Simulizi la polisi nalo ni tofauti huku Kamanda wa Polisi wa Kaunti Ndogo ya Vihiga William Serongo akisema Bw Olwanda alipigwa na umati baada ya mzozo kuibuka ikidaiwa alimdunga mwanaume mwengine Hussein Hassan kwa kisu. “Wananchi walimgeukia baada ya kuona tukio hilo na kumvamia,” akasema Bw Serongo na kuongeza kuwa mwanaume ambaye alidungwa kisu anaendelea kupokea matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Vihiga. Idara ya Upelelezi Nchini (DCI) ilitoa taarifa iliyosema kisu ambacho marehemu alikitumia kilipatikana na kutwaliwa kutoka eneo hilo.