Wamatangi apuuza ‘mgomo’ wa baraza la magavana, afika kwa ukaguzi Seneti

GAVANA wa Kiambu, Kimani Wamatangi alipuuza 'mgomo' wa Baraza la Magavana na kufika kwa Kamati ya Uhasibu inayoongozwa na Seneta Moses Kajwang kuwajibikia hesabu za kaunti yake, jana. Haya yanajiri huku uongozi wa Seneti ukitishia kususia mkutano baina ya Seneti na Baraza la Magavana uliopangiwa kufanyika Alhamisi, Februari 26 kusuluhisha malumbano baina ya asasi hizo mbili za ugatuzi. Bw Wamatangi alihoji kwamba katiba inawatambua magavana wote 47 kama wakurugenzi watendaji wa kaunti hivyo hawana budi kuwajibikia fedha za umma wanazoaminiwa kusimamia. “Kama Gavana wa Kiambu, fasiri yangu ya sheria na katiba ni kwamba jukumu la kuwajibikia rasilimali zinazotengewa watu wa Kiambu ni mahsusi na lipo mikononi mwa serikali ya kaunti na gavana,” alisema Gavana Wamatangi katika kikao cha kamati ya seneti jana. Gavana Wamatangi alieleza Kamati ya Seneti kuhusu Ukaguzi wa Hesabu za Umma (CPAC) kuwa “Katiba inatambua gavana kama mkurugenzi wa kaunti”. “Tafsiri yangu ni kwamba hatuna njia mbadala ila kufika hapa kama serikali ya kaunti na ndiposa niliwaagiza watu wangu tuje hapa ili tushughulikie masuala yaliyoangaziwa na mkaguzi mkuu.” Gavana Wamatangi alisema haya huku uongozi wa seneti ukiapa kutoshiriki mkutano uliopangiwa kufanyika kesho (Jumatano) kwa lengo la kutatua mgogoro unaotokota kati ya maseneta na baraza la magavana (CoG). Mwenyekiti wa CPAC, Seneta Moses Kajwang (Homabay), alisema kwamba uamuzi wa Gavana Wamatangi kufika mbele ya seneti “sio kibali bali wajibu kikatiba". “Isionekane kana kwamba tunawasihi magavana wengine kujitokeza. Ulipoamua kugombea ugavana ulitia saini kuwa mkurugenzi wa kaunti anayewajibika na uwajibikaji ni mtu binafsi huwezi kujificha nyuma ya kundi linalojiita CoG kukwepa uwajibikaji,” alisema Seneta Kajwang. Kulingana na Seneta Kajwang, hakuna changamoto la kikatiba ila watu wachache tu wasiotaka kuwajibikia raslimali za umma, “Sidhani kuna tatizo. Mkutano wa 26 ni kikao tu cha kunywa chai, sio lazima, hautaathiri jinsi kamati hii itakavyoendelea na kazi yake na magavana wanaoelewa katiba watafanya alichofanya Gavana wamatangi,” alisema Kajwang. “Ugatuzi upo hatarini duniani kote na magavana wanalala wakati wa mageuzi. Kwa mfano serikali kuu inapotumia ardhi ya kaunti kujenga makazi ya bei nafuu au uwanja wa spoti, mali hiyo ni nani, kaunti au serikali kuu? Haya ndiyo mazungumzo tunapaswa kushiriki na magavana. Sitaki kuzungumza na magavana kuhusu kuhangaishwa, kuitishwa hongo. Ikiwa madai hayo yangekuwa thabiti EACC ingekuwa imechukua hatua kufikia sasa.” Seneta wa Nandi, Samson Cherargei alisema kwamba uongozi wa seneti “umeamua hatutaenda kushiriki mkutano haramu na CoG” aliyosema “sio taasisi halali yenye msingi kisheria”. Hata hivyo, Gavana Wamatangi aliyehudumu awali kama seneta, alitoa wito kwamba mgogoro kati ya taasisi hizi mbili utasuluhushwa upesi na kwa dharura. “Mihimili miwili thabiti ya ugatuzi ni seneti na CoG. Tumepiga hatua kubwa katika ugatuzi kutokana na kujitolea na juhudi za seneti. Mara nyingi wakati masuala yamezuka hususan kuhusu ugavi wa raslimali, tumekuja kuomba seneti usaidizi.”