Murang’a, Nakuru, Kiambu na Kisumu zaibuka bora katika kubuni ajira

KAUNTI za Murang’a, Nakuru, Kiambu, Kisumu na Meru zimeibuka bora zaidi katika uundaji wa nafasi za ajira, matumizi ya mifumo ya kidijitali na utoaji wa huduma za serikali mtandaoni, kulingana na ripoti mpya iliyotolewa na shirika la serikali la Kenya Vision 2030. Ripoti hiyo iliorodhesha Murang’a katika nafasi ya kwanza kwa asilimia 98.3. Nakuru ilifuata kwa asilimia 87.3, Kiambu 83.9, Kisumu 81.2 huku Meru ikifunga orodha ya tano bora. Kwa upande mwingine, kaunti za Baringo (38.7), Marsabit (38.4), Tana River (35.8), Pokot Magharibi (35.1), Garissa (30.1) na Wajir (28.8) zilipata chini ya asilimia 40. Tathmini hiyo ilichunguza jinsi serikali za kaunti zinavyotumia teknolojia na majukwaa ya kidijitali kuboresha utoaji huduma, kuimarisha ukusanyaji wa mapato na kuchochea uchumi wa maeneo yao. Mkurugenzi Mkuu wa Kenya Vision 2030, Kenneth Mwige, alisema utafiti huo uliangazia maeneo muhimu kama mikakati ya kuunda ajira, kupata huduma mtandaoni kwa haraka, pamoja na usalama na ufanisi wa mifumo ya usimamizi wa mapato. Matokeo yanaonyesha pengo kubwa la maendeleo miongoni mwa kaunti 47 huku chache zikipiga hatua kubwa katika mageuzi ya kidijitali na nyingine zikisalia nyuma kutokana na changamoto za miundombinu na rasilmali. Murang’a ilisifiwa kwa mpango wake kabambe wa dijitali uliobadili kwa kiasi kikubwa utoaji huduma na ukusanyaji mapato. Kupitia mifumo ya kidijitali, kaunti hiyo imeongeza mapato yake ya ndani kutoka chini ya Sh500 milioni hadi zaidi ya Sh1.3 bilioni bila kuongeza ushuru au ada. Aidha, huduma nyingi muhimu kama za hospitali, maombi ya vibali na huduma za kilimo zimehamishwa mtandaoni. Miongoni mwa ubunifu uliotajwa ni mfumo wa Inua Mkulima unaowawezesha wakulima kupokea ruzuku kila robo mwaka kupitia simu zao za mkononi. Pia, maombi ya basari hufanywa mtandaoni na waombaji kufahamishwa kidijitali, jambo linalopunguza urasimu na kucheleweshwa kwa maamuzi. Profesa Kiarie Mwaura, waziri wa fedha kaunti ya Murang’a, alisema kaunti hiyo inalenga kuunganisha huduma zote katika mfumo moja hivi karibuni. Kaunti za Nakuru, Kiambu, Kisumu na Meru pia zilifanya vyema kutokana na uwekezaji katika mifumo ya kupata vibali mtandaoni, ukusanyaji mapato kidijitali na mageuzi ya kiutawala yaliyopunguza mianya ya ufisadi. Kwa mujibu wa takwimu za jumla, kaunti saba zilipata kati ya asilimia 80 na 100, kaunti 17 zikapata kati ya 60 na 79, huku nyingine 17 zikisajili kati ya 40 na 59. Kaunti sita zilipata chini ya asilimia 40, hali inayoashiria mapungufu makubwa katika ukumbatiaji wa dijitali na utoaji huduma. Ripoti ilibainisha kuwa kaunti zilizo katika maeneo kame na nusu kame zinakabiliwa na changamoto za mtandao hafifu, ukosefu wa wataalamu wa teknolojia na bajeti ndogo. Mwige alihimiza kaunti zilizofanya vibaya kuiga mfano wa Murang’a na kurekebisha mikakati hiyo kulingana na mahitaji yao. Aliongeza kuwa dijitali huimarisha uwazi na uwajibikaji katika usimamizi wa fedha za umma kwa kupunguza mawasiliano ya ana kwa ana yanayoweza kuchochea ufisadi. Kaunti zilizokumbatia mifumo ya kidijitali tayari zinashuhudia manufaa kama kuongezeka kwa mapato, kurahisishwa kwa biashara na huduma za haraka kwa wananchi. Hata hivyo, tofauti kubwa zinaonyesha kuwa ahadi ya ugatuzi bado haijatekelezwa kwa usawa, na kaunti zilizo nyuma zinahitaji kuchukua hatua za haraka ili zisizidi kuachwa nyuma.