KATIBU Mkuu wa chama cha Orange Democratic Movement (ODM) Edwin Sifuna, amefichua kuwa wakati wake ndani ya chama hicho kikubwa cha upinzani unakaribia kuisha, huku akielezea uwezekano wa kujiunga na muungano wa upinzani. Kauli hiyo inaashiria kuwa mjadala wa “wantam” unaoendelezwa na vuguvugu la Linda Mwananchi na Muungano wa Upinzani umepangwa kufanikisha lengo la kumshinda Rais William Ruto katika uchaguzi mkuu ujao. Akizungumza katika kipindi cha Fixing The Nation cha runinga ya NTV, Sifuna alisema anafuatilia mirengo mingine iliyo na ajenda sawa ya kuondoa Rais William Ruto katika uchaguzi mkuu wa 2027. “Tunahitaji kuonyesha kwa nguvu kwamba, hatutavumilia utawala wa William Ruto na yote anayoyasimamia. Tunapaswa kumshinda kwa angalau kura milioni tano. Hii ni ishara ya wazi kwamba, wananchi wanakataa aina hii ya utawala, na itakuwa funzo kwa taifa zima,” alisema Seneta Sifuna. Akikiri kuwa kumshinda Rais Ruto hakutakuwa kazi rahisi, Sifuna alitoa wito kwa upinzani kuungana katika kampeni ya kuhakikisha Ruto hatapata muhula wa pili, ili kuziba mianya ya kuiba kura. Alisema hakuna yeyote anayefaa kudhani kuwa kuondoa rais anayehudumu ni jambo rahisi bila mipango makini, ikiwemo kuungana na wanasiasa wengine wenye ushawishi. “Tunapaswa kukubaliana kuwa nguvu zake si kidogo. Lazima tuchague mkakati wa pamoja ambao utahakikisha tunamfanya rais aondoke Ikulu,” alisema Sifuna. Seneta huyo alieleza kuwa mikutano ya Linda Mwananchi itatumika kama kielelezo cha hatua zijazo. Pia aliwataka wafuasi wake kujisajili kwa wingi kushiriki katika uchaguzi ili kuhakikisha wana nguvu za kisiasa. Alisisitiza kuwa hofu na vitisho vinavyotolewa na baadhi ya viongozi wa kisiasa havitayumbisha wananchi wala kuharibu haki zao za kikatiba kushiriki katika siasa. Pia alikanusha madai kuwa Rais (mstaafu) Uhuru Kenyatta anafadhili mikutano yao, akisisitiza kuwa mikutano hiyo inatokana na hamu ya wananchi kutaka uongozi mbadala. “Hii si kuhusu pesa, bali ni kuhusu mapenzi mema ya wananchi. Tumepokea maelfu ya jumbe na ushauri kutoka kwa wananchi wanaotaka kujiunga na vuguvugu la Linda Mwananchi,” alisema Sifuna. Bw Sifuna pia alikanusha madai ya DCI na Waziri wa Usalama wa Ndani Kipchumba Murkomen kwamba, ni mrengo wao uliorusha vitoza machozi katika uwanja wa Amalemba, Kakamega, akisisitiza kuwa vijana walitambua watu waliokuwa wakizua vurugu. Alisema kama viongozi hawangeingilia kati watu hao wangeuawa. Akisema anatiwa nguvu na wafuasi wanaomtambua kwa uongozi wake, Seneta huyo alisema itakuwa makosa kuonyesha anamiliki vuguvugu hilo. Seneta Sifuna alisisitiza umuhimu wa upinzani kuungana ili kuhakikisha wananchi wanapata viongozi wanaojali masilahi yao. Alisema kuwa upinzani ukiungana, unaweza kumnyima Rais Ruto fursa ya kuendelea kukaa Ikulu, akionyesha mpango wa kisiasa wa kuunganisha wanachama wa ODM walio na ajenda sawa na wanasiasa wengine wa upinzani. “Hatuwezi kumshinda peke yetu bila umoja. Hii ndio sababu tuko tayari kujiunga na wanasiasa wengine ambao wana ajenda sawa ya kuondoa utawala usiojali mahitaji ya wananchi,” alisema. Kauli ya Sifuna pia inaonyesha kuwa anaandaa mikakati ya kisiasa ya muda mrefu na kwamba, kila anayelenga kumshinda Rais Ruto lazima alindwe dhidi ya vitisho vyovyote kutoka kwa wale wanaopinga demokrasia. Mvutano ndani ya ODM unaonyesha kuwa baadhi ya viongozi hawaridhiki na mpango wa chama kuwa na mkataba na UDA kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027.