FESTUS Arasa Omwamba, 33, ametajwa kama mmoja wa watu wanaotafutwa zaidi na maafisa wa usalama kufuatia madai mazito yanayomhusisha na kuwasafirisha Wakenya kupigana katika vita vya Urusi dhidi ya Ukraine. Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Ujasusi la Taifa (NIS) iliyowasilishwa bungeni Februari 18, 2026, amri ilitolewa Omwamba azuiwe kusafiri nje ya nchi kwa madai ya kushawishi takriban Wakenya 1,000 kujiunga na jeshi la Urusi. Inadaiwa kampuni yake, Global Face Human Resource Ltd, ilifanya kazi bila leseni kutoka Mamlaka ya Kitaifa ya Ajira na kushirikiana na watu walio Moscow kusaka vijana wa Kenya. Ripoti hiyo inasema mbali na kuwatafuta vijana, kampuni hiyo iliwasaidia kupata malazi wakisubiri safari na kufungua akaunti za benki kupokea bonasi ya kujiunga iliyodaiwa kuwa kati ya Sh910,000 na Sh1.2 milioni. Hata hivyo, Omwamba ambaye ni mwanachama aliyesajiliwa wa chama tawala cha UDA aliambia ‘Taifa Leo’ akiwa Urusi kuwa amekuwa akifanya kazi kama msimamizi katika kampuni ya usafi na atarejea Nairobi katikati ya Machi. Alikanusha kuhusika na kuwasafirisha vijana vitani, akidai baadhi yao walijiunga kwa hiari. Wakati huo huo, mahakama kuu iliagiza DCI kuchunguza madai ya jaribio la ulaghai ambapo Omwamba na kampuni yake walituhumiwa kujaribu kunufaika na akaunti ya benki ya mtu aliyefariki mwaka mmoja kabla ya kesi kufunguliwa.