Baada ya kuhangaishwa na kiangazi, wakazi sasa wahofia mafuriko

SERIKALI ya Kaunti ya Tana River, inataka maandalizi yafanywe mapema kuepuka athari za mafuriko huku eneo hilo likiendelea pia kukumbwa na makali ya ukame. Gavana wa Tana River, Bw Dhadho Godhana, alisema mvua inayonyesha katika maeneo ya milimani nchini, huenda ikachangia mafuriko katika nyanda za chini. Katika taarifa iliyotolewa Jumanne, Februari 24, Idara ya Utabiri wa Hali ya Hewa nchini ilisema kuwa, mvua ingeendelea kushuhudiwa katika sehemu kadhaa nchini, ikiwemo eneo la Kati, Nyanza, Bonde la Ufa, Nyanda za chini za Kusini Mashariki, sehemu za Pwani, Magharibi na Kaskazini Magharibi. Taarifa ya awali iliyotolewa Februari 20 ilikuwa imetaja Kaunti ya Tana River miongoni mwa kaunti za Pwani ambazo zingeathirika na mafuriko, licha ya kukosa mvua kubwa. “Mafuriko yanaweza kutokea hata katika maeneo ambayo mvua kubwa haijashuhudiwa, haswa maeneo yaliyo katika nyanda za chini ama inakoelekea mito. Tunaomba umma kutahadhari na kutoendesha gari wala kutembea katika maji yanayosonga au katika maeneo yaliyofurika,” ikasema tahadhari hiyo. Athari za aina hiyo ya hali ya hewa tayari imeanza kuhisiwa Kaunti ya Narok, ambako Mamlaka ya Barabara Kuu nchini imewaonya madereva kuhusu daraja la Mogor lililobomoka katika barabara inayounganisha miji ya Kilgoris na Lolgorian. Akizungumza akiwa Chewani, Gavana Godhana alisisitiza umuhimu wa serikali ya kitaifa, ya kaunti, na wadau wengine kuungana ili kukabiliana na mafuriko ambayo huenda yakaathiri maisha wakati wa misimu kama hiyo. “Tuko kwenye hatari kwa mujibu wa wataalamu. Wametuambia kuwa kuna mvua kidogo hapa lakini mvua nyingi kule bara. Kwa hivyo tunatarajia kuwa kutakuwa na mafuriko huku ambako mito inaelekea na tunapaswa kujitayarisha,” akasema Gavana Godhana. Alieleza kuwa, mbinu ya kujumuisha taasisi mbalimbali kushughulikia kiangazi na mafuriko hayo ingehakikisha kuwa wakazi wanalindwa ilhali kuna uwajibikaji wa njia zilizotumika kushughulikia matatizo hayo. Aliongeza kuwa serikali yake, pamoja na serikali ya kitaifa zilikuwa zikiendelea na ugavi wa chakula cha msaada kwa wakazi wa Tana River kuwasaidia kukabiliana na makali ya njaa yanayosababishwa na kiangazi hicho. “Tayari kuna chakula kinasambazwa, maji pia yanasambazwa na magari ya kusafirisha maji katika maeneo mbalimbali. Tunasubiri kupata chakula zaidi na bidhaa zingine muhimu,” akasema Gavana Godhana. Aliongeza kuwa washikadau wengi ikiwemo serikali kuu, serikali ya kaunti, Shirika la Msalaba Mwekundu, Mamlaka ya kukabiliana na Kiangazi (NDMA) na washirika wengine walikuwa wakiungana kukabiliana na majanga hayo kwa wakati mmoja.