Mko peke yenu, maseneta waambia magavana katika ari ya kudai Sh535 bilioni kwa Serikali

MASENETA wamejitenga na magavana katika msimamo wao wa kudai Sh534.96 bilioni kama mgao wa kaunti katika mwaka wa kifedha utaomalizika Juni 2027. Hatua hii inafuatia pendekezo la Kamati ya Seneti ya Fedha na Bajeti kwamba kaunti zigawiwe Sh454.74 bilioni, hili likiwa pengo la Sh80.2 bilioni ikilinganishwa na pesa ambazo Baraza la Magavana (CoG) linataka. Pendekezo hilo la kamati inayoongozwa na Seneta wa Mandera, Ali Roba, pia ni la chini kuliko la Mamlaka la Ugavi wa Mapato (CRA), ambayo imependekeza Wizara ya Fedha itenge angalau Sh458.94 bilioni kwa kaunti. Haya yanajiri wakati ambapo maseneta na magavana wanavutana kuhusu mahudhurio ya vikao vya kamati za uangalizi za Seneti kutoa maelezo kuhusu matumizi ya mabilioni ya fedha zinazotengewa kaunti. Katika mwaka wa fedha wa sasa unaoisha Juni 30, 2026, kaunti 47 zilitengewa Sh415 bilioni kama mgao sawa wa mapato. Kamati ya Seneti ilisema baada ya kuzingatia Taarifa ya Sera ya Bajeti na maoni ya wadau, inapendekeza mgao wa Sh454,743,15,879 kwa mwaka wa fedha 2026/27. CoG, chini ya mwenyekiti wake Ahmed Abdullahi, ilihimiza kamati hiyo kuunga mkono pendekezo la magavana la Sh534.96 bilioni, baada ya serikali ya kitaifa kupendekeza kaunti zipokee Sh420 bilioni pekee kuanzia Julai mwaka huu — ongezeko la Sh5 bilioni tu ukilinganisha na mwaka wa kifedha unaoisha Juni 30. Pendekezo la magavana linajumuisha nyongeza ya Sh106.97 bilioni, ikiwemo Sh35 bilioni kutokana na ukuaji wa mapato na Sh8.94 bilioni za kuwaajiri wahudumu wa afya walioajiriwa chini ya mpango wa UHC kwa masharti ya kudumu na pensheni. Pia wanataka Sh65.97 bilioni kwa majukumu yaliyogatuliwa lakini bado yanatekelezwa na wizara na idara za kitaifa. Hata hivyo, baadhi ya maseneta wameonya kuwa hawataunga mkono ongezeko hilo iwapo magavana wataendelea kususia kamati za uangalizi. Mwenyekiti wa Kamati ya Seneti ya Hesabu za Kaunti (CPAC), Moses Kajwang', alisema magavana lazima kwanza wawasilishe matumizi ya Sh387 bilioni walizopokea mwaka wa fedha uliomalizika Juni 30, 2025. Aliongeza kuwa Seneti haiwezi kuamrishwa na CoG jinsi ya kuendesha shughuli zake mradi inafuata sheria. Seneta wa Kitui Enoch Wambua na Seneta wa Nandi, Samson Cherargei walisisitiza kuwa kufika mbele ya Seneti ni wajibu wa kikatiba, si hiari. Mvutano huu unatarajiwa kuathiri mchakato wa kupitisha mgao wa fedha kwa kaunti huku kila upande ukishikilia msimamo wake kuhusu uwajibikaji na mgao wa rasilimali. Baadhi ya maseneta wamesema kuwa iwapo magavana wataendelea kususia kamati za uangalizi, hawataunga mkono ongezeko lolote la bajeti. Hii inaweza kusababisha kuchelewa kwa utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika kaunti zote 47. Aidha, maseneta wamesisitiza umuhimu wa uwajibikiaji wa fedha za umma, wakisema kuwa hakuna sababu ya magavana kutaka waongezewe mapato kabla ya kuwajibikia walivyotumia Sh387 bilioni walizopewa.