GAVANA wa Mombasa, Bw Abdulswamad Nassir, ameagiza akina mama zaidi ya 100 waliokuwa wamezuiliwa katika wodi ya kujifungua katika Hospitali Kuu ya Rufaa ya Pwani waachiliwe pamoja na watoto wao. Wanawake hao walikuwa wamezuiliwa kwa kushindwa kugharamia ada za matibabu zinazofika jumla ya karibu Sh100,000, na hawakuwa wamejisajili katika bima ya afya ya SHA. “Tuliambiwa hatuwezi kuondoka hadi pale tutakapolipia gharama za matibabu. Nikaamua kuanza maisha kwenye hospitali hii na mtoto wangu mchanga. Nilikuwa nafanya biashara ya kuuza sharubati,” alisema Bi Vynonne Nyaga ambaye alikuwa amekaa kwenye hospitali hiyo kwa muda wa mwezi mmoja. Hospitali hiyo inakumbwa na changamoto mbalimbali ikiwemo uhaba wa wahudumu, rasilimali, na mazingara duni ya utendakazi. Meneja wa idara ya uuguzi Roda Usui, alisema msongamano katika wodi ya kina mama huwa ni hatari hasa kwa watoto wachanga ambao wanaweza kuambukizwa maradhi mengine pamoja na mama zao hivyo basi kuathiri huduma za afya.