MVUTANO mkali umeibuka kati ya Msimamizi wa Ikulu, Katoo Ole Metito, na Wizara ya Fedha kuhusu kucheleweshwa kwa malipo ya pensheni ya aliyekuwa Makamu wa Rais Moody Awori pamoja na marupurupu ya mjane wa aliyekuwa Makamu wa Rais marehemu George Saitoti. Akizungumza mbele ya Kamati ya Bunge kuhusu Utawala na Usalama wa Ndani, Bw Ole Metito alifichua kuwa Wizara ya Fedha imetatiza juhudi zake za kuhakikisha Bw Awori anapata pensheni yake kwa mujibu wa sheria. Alisema ameandika barua kadhaa akiomba fedha hizo zijumuishwe katika bajeti ya Ikulu lakini hajapokea majibu yoyote. “Tumeandikia Wizara ya Fedha barua kuomba itenge fedha inavyotakiwa kisheria, lakini hatujapata majibu. Sijui sababu ya kucheleweshwa huku,” alisema Ole Metito huku akiwasilisha nakala za barua hizo kwa kamati. Ikulu, ambayo afisa wake mkuu wa uhasibu ni Msimamizi, husimamia marupurupu ya marais wastaafu, manaibu wao na maafisa wengine walioteuliwa, kulingana na mgao wa Bunge. Sheria ya Marupurupu ya Kustaafu ya Naibu Rais na Maafisa Wengine Walioteuliwa inatoa haki ya pensheni na mafao mengine kwa waliowahi kuhudumu kama Naibu Rais, Waziri Mkuu, Makamu wa Rais, Spika, Naibu Jaji Mkuu au Jaji Mkuu baada ya Januari 1, 1993.