Muda wa ‘ndoa’ ya ODM na UDA uliwekwa kutamatika Machi 7, asema Orengo

GAVANA wa Siaya, James Orengo, amesema mkataba wa kisiasa kati ya Orange Democratic Movement (ODM) na chama cha Rais William Ruto utaisha Machi 7, 2026 na akataka tathmini ya makubaliano yaliyozaa Serikali Jumuishi. Mwanasiasa huyo mkongwe, ambaye hivi majuzi alionekana kuegemea mrengo wa ODM wa Linda Mwananchi unaoongozwa na Katibu Mkuu Edwin Sifuna, alisema chama hicho kitafanya mkutano jijini Nairobi Machi 7 pamoja na wenyeviti wa kanda ili kupitia makubaliano ambayo anadai hayajatekelezwa kikamilifu. Mkataba huo wa vipengele 10 ulitiwa saini na Rais William Ruto na aliyekuwa kiongozi wa ODM marehemu Raila Odinga mnamo Machi 8, 2025. Makubaliano hayo yalilenga kuimarisha umoja wa kitaifa na ustawi wa nchi. Yalipendekeza utekelezaji wa ripoti ya Kamati ya Mdahalo wa Kitaifa (NADCO), kukuza ujumuishaji katika utawala na maendeleo ya taifa, kulinda na kuimarisha ugatuzi, pamoja na kushughulikia mzigo wa deni la Kenya. Aidha, yalilenga kuimarisha uadilifu katika uongozi wa kitaifa, kukomesha ubadhirifu wa rasilmali za umma, kupambana na ufisadi, kulinda haki ya kukusanyika kwa amani, na kuheshimu utawala wa sheria na katiba. “Tutathmini utekelezaji wa makubaliano. Ninapozungumza sasa, wengi wetu tunajua makubaliano hayo hayajatekelezwa. Tarehe 8 tutafanya mkutano mkubwa katika viwanja vya Jacaranda jijini Nairobi kama mkutano wa kwanza, kisha kufuatiwa na mikutano mingine kote nchini kuwaelimisha wafuasi wa ODM,” alisema Orengo. Aliongeza: “Hiki ndicho chama kinachoitwa ODM. Tunataka kibaki kikiwa kimeungana. Tunataka umoja na uadilifu wa chama ulindwe, si tu kwa miaka 20 ambayo Raila Odinga alikuwa hai, bali kwa vizazi vijavyo.” Orengo alikuwa akizungumza katika mkutano wa faragha na baadhi ya viongozi wa ODM wa kaunti wanaounga mkono mrengo wa Linda Mwananchi uliofanyika Ong’ata Rongai, Kaunti ya Kajiado.