Uvimbe katika mishipa ya korodani ndio husababisha ugumba, Watafiti wasema

W ATAALAMU wamebaini kuwa uvimbe wa mishipa kwenye korodani ndio huchangia zaidi mwanaume kuwa gumba. Uvimbe huo wa mishipa usipogunduliwa mapema hasa wakati wa utineja, basi huchangia kupunguza uzalishaji wa mbege za kiume na kuathiri kutoka kwao sehemu moja hadi nyingine. Wengi wa wanaume wanaosumbuliwa kuwatungisha wake zao mimba, mara nyingi hubainika kuwa na tatizo hili la uvimbe wa mishipa. Chanzo cha mwanaume kuwa gumba hutokana na mabadiliko kwenye kiwango cha shahawa kinachozalishwa, tatizo la mbegu za kiume kutoka sehemu moja hadi nyingine kisha mbegu za kiume kuwa chache wakati wa kushiriki mapenzi. Pia kuharibiwa kwa chembechembe za DNA kunaweza kuzuia mbegu za kiume na kike kukutana kisha kuzuia kuanza mchakato wa kuundwa kwa mtoto tumboni. Dkt Bobby Najari kwenye jarida la afya la NYU Langone, anasema tatizo la uvimbe kwenye korodani sasa lipo sana kutokana na masuala mbalimbali yanayoathiri afya ya uzazi kwa wanaume. Unene kupita kiasi, athari za mazingira ambapo mwanaume anaishi pamoja na magonjwa ya kuambukizana wakati wa ngono pia huchangia mwanaume kuwa gumba. Dkt Najari anasema kuwa njia bora zaidi ya kuzuia mwanaume kuwa gumba ni mtaalamu wa afya kupima shahawa. “Kipimo hicho kitabaini iwapo mbegu za kiume zipo kiasi cha chini na pia itafahamika kiwango cha homoni za kiume ambazo huashiria korodani ianze mchakato wa kuzalisha mbegu za kiume,” akasema mtaalamu huyo. Dkt Najari anaongeza kuwa tatizo la ugumba linaweza kusuluhishwa kupitia upasuaji au kubadilisha mtindo wa maisha. Kwa kiasi kikubwa, unene kupita kiasi ndio husababisha matatizo mengi ya uzazi kwa wanaume. Kuwa na mafuta mengi mwilini ndio huchangia homoni ya kiume kubadilishwa kuwa estrojeni ambayo husababisha ugumba.