KWA jina la Mwenyezi Mungu mwenye kuneemesha neema kubwa kubwa na neema ndogo ndogo, ni fahari kubwa kwamba tunakutana kwenye ukumbi huu Ijumaa hii ya pili ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhan. Mwanzo tuanze kwa kumshukuru mno Muumba wetu Subuhaanahu wata’ala, mwingi wa rehema na muumba wa mbingu na ardhi na vyote vilivyomo. Hakika hapana mwingine anayestahili kuabudiwa, kuenziwa ila ni Allah (SWT) pekee. Baada ya kumshukuru Allah (SWT) wetu, pia tuchukue muda huu wa kipekee kumtakia kheri, kumtilia dua na kumfanyia maombi Mtume wetu (SAW). Ndugu yangu natumai saum inakupeleka vizuri mbali na changamoto mbalimbali ambazo zimekuwepo katika baadhi ya maeneo nchini. Kwa mfano ndugu zetu kutoka Kaskazini Mashariki na baadhi ya sehemu za Pwani wamekuwa wakilalamikia ukosefu wa maji msimu huu wa Ramadhan. Tunaomba serikali na idara husika ziingilie kati ili waumini wapate maji wa kutumia kushika wudhu kabla ya swala pamoja na matumizi mengine ya kawaida. Leo nitabadilisha gia na kubadilisha ukumbi huu kuwa wa mafunzo hasa kwetu waumini wanaoendelea kufunga. Katika pitapita zangu niliwasikia baadhi ya waumini wakipiga gumzo iwapo ni sawa kuanza kufunga bila kula suhoor (mlo wa asubuhi kabla ya kuanza kufunga). Hii ni kwa sababu wakati mwingine baadhi yetu huamka na kuswali kisha kurudi usingizini wakisema hawana njaa ama wengine baada ya kula usiku hawaamki asubuhi kuswali na kuendelea kufunga tu siku nzima. Kuna baadhi ya watu waliokuwa wakisema ni sawa lakini wapo wengine waliokuwa wakipinga. Mwanzo ni vyema ifahamike hatuli suhoor kwa sababu ya njaa bali tunaila kwa sababu ni ibada na ni chakula ambacho kimebarikiwa. Pia tunakula suhoor kwa sababu wakati huo huwa umebarikiwa. “Suhoor ni mlo ambao umebarikiwa, kwa hivyo, usiuache hata kama mmoja wenyu anapiga tu funda la maji. Hii ni kwa sababu Allah (SWA) na malaika wake hutuma shifaa kwa wale ambao hula suhoor,” ikasema Hadith ya Mtu Mohammed (SWT) ilivyosimuliwa na Ahmad. Kwa hivyo, sote tule suhoor hata kama ni tende pekee yake au kunywa maziwa tusikose baraka. “Suhoor ambayo imebarikiwa zaidi ni tende,” akasema Mtume Mohamed (SWT). Ibada ya saum nayo ni muhimu zaidi ya kushinda njaa na kiu pamoja na matamanio ya nafsi. Ibada hii inafaa kumjenga mtu kwa takwa yake, takwa ambayo ni mlango mpana na kuangalia maamrisho ya Allah na makatazo yake. Saum si ya kudhoofisha mwili bali ni kuimarisha uhusiano na Allah na kujijenga sana kiimani. Kwa hivyo, kufunga bila kuswali ni kazi bure na anayefanya hivyo hatakuwa akifuata amri ya Allah wakati huu wa Ramadhan.