Moshi. Zikiwa zimepita siku saba baada ya Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba kuagiza Chama Kikuu cha Ushirika Mkoa wa Kilimanjaro (KNCU) kuuza moja ya mali zake ili kulipa deni la zaidi ya Sh400 milioni kwa vyama vya msingi 12, utekelezaji wa agizo hilo umeanza huku Sh225 milioni zikilipwa kwa vyama vinane. Madeni hayo yanatokana na mauzo ya kahawa yenye uzito wa kilo 40,283 yaliyouzwa kupitia KNCU, lakini chama hicho hakikulipa malipo ya vyama hivyo tangu mwaka 2023. Akizungumza leo Februari 27, 2026 katika kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC), Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu amesema malipo yaliyosalia ya Sh185.9 milioni kwa vyama vinne yatalipwa Machi 6, 2026. “Kuna vyama vya msingi 12 vilivyokuwa vinadai jumla ya Sh412 milioni, napenda kuwafahamisha kuwa, vyama nane tayari vimeshalipwa fedha zao na zimeingizwa kwenye akaunti zao, kati ya hivyo, vyama vinne vimepata Sh33.8 milioni na vingine vinne Sh192.37 milioni,” amesema Babu. Awali, Februari 20, 2026, Dk Mwigulu akiwa katika ziara mkoani Kilimanjaro eneo la Chekereni, Njia Panda, Wilaya ya Moshi, alipokea malalamiko ya vyama vya msingi vilivyodai kutolipwa fedha zao za kahawa kwa zaidi ya miaka mitano. Mmoja wa viongozi wa Chama cha Msingi cha Mwika Kinyamvuo, Glory Sam, alimweleza Waziri Mkuu kuwa tangu msimu wa mwaka 2021/22 walipowasilisha kahawa yao kupitia KNCU, hawajapata malipo ya mabaki wala nyongeza. “Tulikuwa vyama vya msingi 11, tulipeleka kahawa yetu KNCU mwaka 2021/22, lakini tangu hapo hatujalipwa mabaki wala nyongeza. Tumezungushwa tangu mwaka huo. Nimefika hadi Dodoma kwa Mrajis Mkuu wa Vyama vya Ushirika , lakini hatukupata mafanikio,” amesema Glory Sam. Pamoja na mambo mengine, amesema kwa mwaka wa fedha 2026/27 halmashauri zote za mkoa huo zimepanga kutumia Sh398 bilioni kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo, mishahara pamoja na matumizi mengine. Katibu Tawala wa mkoa huo, Kiseo Nzowa amewataka viongozi wa mkoa huo kuwa wamoja na kuwajibika kwa wananchi na kushughulikia migogoro inayowakabili. “Viongozi ambao hawana mawasiliano mazuri wabadilike muwe wamoja, mshikamano ni jambo muhimu sawa, kwa yale maeneo ambayo viongozi wanaonekana hawana maelewano, mkae pamoja na kufanya kazi pamoja ili muweze kukaa na kutatua changamoto za wananchi kwenye maeneo yenu,” amesema Nzowa.