Kamishna: Nidhamu, uadilifu ni msingi wa polisi

Morogoro. Jumla ya askari 785 wa Jeshi la Polisi wamehitimu mafunzo ya uongozi mdogo katika Chuo cha Maofisa wa Polisi Kidatu, huku wahitimu hao wakitakiwa kuzingatia haki za binadamu, nidhamu na uadilifu wanapotekeleza majukumu yao ya kazi. Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo yaliyowahusisha askari wa vyeo vya Sajini Meja (SM), Sajini Staff (SSGT) na Sajini (SGT), jana Februari 26, 2026, wilayani Kilombero, Kamishna wa Polisi Zanzibar, Kombo Khamis Kombo, amesema kuwa uongozi wa ngazi ya sajini una nafasi kubwa katika kusimamia utendaji wa kila siku wa Jeshi la Polisi. Ameeleza kuwa sajini ndio kiungo muhimu kati ya uongozi wa juu wa jeshi na askari waliopo mstari wa mbele, pamoja na wananchi wanaohudumiwa na Jeshi la Polisi. Kamishna Kombo amesema askari hao wanapaswa kuwa mfano wa kuigwa kwa matendo yao, hasa katika kusimamia haki za binadamu, kuimarisha misingi ya utawala bora na kujiepusha na vitendo vya rushwa. Amebainisha kuwa, mwenendo wa viongozi wa ngazi ya chini una mchango mkubwa katika kujenga au kubomoa imani ya jamii kwa Jeshi la Polisi. Katika hafla hiyo, Kamishna Kombo alikagua gwaride la wahitimu, kutoa zawadi kwa askari waliofanya vizuri zaidi katika mafunzo hayo, pamoja na kushuhudia maonesho mbalimbali yaliyoandaliwa kama sehemu ya kuonesha ujuzi walioupata wakati wa mafunzo. Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Dustan Kyoba amewataka wahitimu kuzingatia misingi minne ya Jeshi la Polisi ambayo ni nidhamu, haki, weledi na uadilifu. Amesema misingi hiyo ndiyo nguzo muhimu katika kulinda amani na usalama, pamoja na kuimarisha utawala wa sheria ndani ya jamii. Awali, akitoa taarifa ya mafunzo hayo, Mkuu wa Chuo cha Polisi Kidatu, Zarau Mpangule amesema kati ya wahitimu hao, wanawake ni 124 na wanaume 661. Mpangule amesema askari hao wamepata mafunzo kwa muda wa miezi mitatu, yakihusisha masomo ya sheria, uongozi, polisi jamii, huduma bora kwa mteja pamoja na mafunzo ya medani za kivita. Ameeleza kuwa mafunzo hayo yamelenga kuongeza ufanisi, uwajibikaji na weledi katika utekelezaji wa majukumu ya Jeshi la Polisi.