Upinzani walemewa katika uchaguzi mashinani

CHAMA tawala cha United Democratic Alliance (UDA) kililemea upinzani na kushinda viti vinne katika uchaguzi mdogo uliofanyika Alhamisi katika maeneo mbalimbali nchini. Katika matokeo yaliyotangazwa naTume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kupitia maafisa wasimamizi wa uchaguzi katika maeneo husika na kuchapisha kwenye tovuti yake, UDA ilishinda viti vyote. Chama hicho kinachoongozwa na Rais William Ruto kilishinda kiti kimoja cha ubunge na viti vitatu vya udiwani. Katika kinyang’anyiro cha kiti cha ubunge Isiolo Kusini, mgombea wa UDA, Tubi Mohammed Tubi, alitangazwa mshindi baada ya kupata kura 7,352. Alimshinda dada yake, Bina Tupi, aliyewania kwa tiketi ya Jubilee na kupata kura 634. Isack Fayo wa National Economic Development Party, ambaye alikuwa amejiondoa kwenye kinyang’anyiro, alipata kura 44. Kiti hicho kilibaki wazi kufuatia kifo cha aliyekuwa Mbunge wa eneo hilo, Mohammed Tupi. Katika Kaunti ya Embu, wagombeaji wa UDA waliibuka washindi kaika chaguzi ndogo zilifanyika katika wadi za Evurore na Muminji, Mbeere Kaskazini. Katika wadi ya Evurore, Duncan Muratia wa UDA alipata kura 7,853, akifuatiwa na Albert Muchira wa Democratic Party aliyepata kura 1,940, huku mgombea huru Johnson Mukuru Mate akipata kura 1,753. Hali ilikuwa sawa katika wadi ya Muminji ambapo Peterson Njeru wa UDA alipata kura 3,207 na kumshinda Boniface Kariuki wa Development Empowerment Party (DEP) aliyepata kura 2,232. Katika Wadi ya West Kabras, Kaunti ya Kakamega, mgombea wa UDA Elphas Shalakha alipata kura 3,317 na kushinda kiti hicho. Bramwel Wasike Khaemba wa Democracy for the Citizens Party (DCP) alipata kura 2,640, huku wagombea wengine wakipata kura chache. Rais William Ruto na Naibu Rais Kithure Kindiki walisherehekea ushindi huo, wakisema ni ishara ya imani wananchi waliyo nayo kwa chama hicho. Rais alisema ushindi huo unaimarisha azma ya kujenga chama cha kitaifa kitakachofanya Kenya kustawi. Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi pia aliipongeza UDA, akisema ushindi huo ni sauti ya wananchi kupitia kura. Wachambuzi wa siasa wanasema kuwa ingawa uchaguzi mdogo wa Alhamisi, ulikuwa wa viti9 vichache tu, uzito wake kisiasa ulikuwa mkubwa sana. Chama cha United Democratic Alliance (UDA) kilisherehekea kile kilichoita “maamuzi ya nguvu,” huku Muungano wa Upinzani ukibaki na maswali magumu kuhusu mkakati wao dhidi ya Rais William Ruto. Katibu Mkuu wa UDA Hassan Omar, alisema matokeo hayo hayakuwa tu ushindi wa maeneo husika bali ulikuwa ujumbe wa kisiasa. Alisema wapigakura wamekataa siasa za maneno matupu na badala yake wanaunga mkono sera zenye mwelekeo. Takwimu zinaonyesha kuwa kati ya chaguzi ndogo 28 zilizofanyika tangu 2022, vyama vinavyounga mkono serikali ya sasa vimeshinda viti 22, jambo ambalo UDA inalchukulia kama thibitisho la ubabe wake wa kisiasa. Viongozi wakuu serikalini walijitosa kikamilifu katika kampeni, akiwemo Naibu Rais Kithure Kindiki aliyepiga kambi Mlima Kenya kabla ya kura. Hii ilitafsiriwa kama mkakati wa kuimarisha ngome ya Rais Ruto katika eneo hilo. Hata hivyo, wachambuzi wanaonya kuwa idadi ndogo ya wapigakura inatia doa ushindi mkubwa. Katika baadhi ya vituo vya kupigia kura Isiolo Kusini, idadi ya waliojitokeza ilikuwa chini ya asilimia 20 kufikia adhuhuri, huku sababu zikihusishwa na Ramadhani, ukame na hali ya kutojali siasa. Kwa upinzani, matokeo haya ni onyo wachukue tahadhari kuelekea 2027. Migawanyiko ya vyama na ukosefu wa uratibu madhubuti vimetajwa kama changamoto kuu. Wakili Chris Omore anasema chaguzi ndogo huathiri taswira ya kisiasa.