CHAMA cha United Democratic Alliance (UDA) kimeweka wazi kuwa wadhifa wa Naibu Rais si ya kujadiliwa katika mazungumzo yake ya kisiasa na Orange Democratic Movement (ODM) kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2027. Katibu Mkuu wa UDA, Hassan Omar, alisema chama hicho tayari kimemuidhinisha Kithure Kindiki kama mgombea mwenza wa Rais Ruto mwaka 2027, akipuuzilia mbali matakwa ya ODM kutaka wadhifa huo kama sehemu ya mazungumzo. “Kama UDA, Naibu Rais Kithure Kindiki ndiye mgombea mwenza 2027. Hatuwezi kuachilia wadhifa huo,” alisema Omar. “Tunasikiliza maoni ya kila mtu, lakini hatutaacha msimamo wa chama.” Kauli hiyo ilijiri wakati ambao Prof Kindiki alikuwa akihudhuria hafla Homa Bay, ngome ya ODM, ambapo baadhi ya vigogo wa chama hicho waliepuka kuzungumzia wazi suala la mgombea mwenza licha ya kiongozi wao Oburu Oginga kunukuliwa akisema wadhifa huo unapaswa kujadiliwa. Katika mkutano huo, viongozi wanaounga mkono serikali jumuishi walirai eneo la Nyanza kumuunga mkono Rais Ruto kwa muhula wa pili. badala ya masharti ambayo ODM ilitangaza mapema wiki hii. Gavana wa Homa Bay Gladys Wanga, ambaye awali alisema ODM itataka mgombea mwenza na asilimia 50 ya nyadhifa serikalini iwapo Ruto atakuwa mgombea, hakuzungumzia suala hilo Ijumaa. Badala yake, alisisitiza umuhimu wa ushirikiano na kusema chama chake kinataka kuwa serikalini. Kiongozi wa Wachache katika Bunge la Taifa Junet Mohamed pia alihudhuria lakini hakuzungumzia wazi suala la mgombea mwenza. Akihutubia umati, Prof Kindiki alisema Rais Ruto atahudumu mihula miwili na kuwaomba viongozi wa ODM kuunga mkono ajenda ya maendeleo. “Muhula mmoja ni nadharia tu. Mihula miwili ni utekelezaji wa miradi ya kuonyesha,” alisema. Aliongeza kuwa serikali jumuishi haimbagui yeyote na kuwa kuna nafasi kwa jamii zote kushiriki katika uongozi na maendeleo ya taifa. Alimnukuu aliyekuwa kiongozi wa ODM Raila Odinga akisema chama hicho kinapaswa kuunga mkono serikali. Kwa upande wake, Dkt Oburu alisema ushirikiano wa sasa unapaswa kuendelea hadi 2027 lakini akaongeza kuwa ODM lazima ijiandae kwa uchaguzi ujao. “Tunataka kujadiliana tukiwa na nguvu, si udhaifu,” alisema, akisisitiza kuwa chama hicho hakijagawanyika kama inavyodaiwa.