Arusha. Wakati matokeo ya mitihani na ubora wa elimu vikiendelea kuwa kipimo cha ufanisi wa shule, wito umetolewa kwa wakuu wa shule za sekondari nchini kuongeza tija, uwajibikaji na ubora wa utoaji elimu katika taasisi wanazosimamia. Wito huo umetolewa leo Februari 27,2026 na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu (ADEM) Dk Maulid Maulid wakati akifunga mafunzo ya siku tatu yaliyohusisha wakuu wa shule na viongozi wa elimu wa Wilaya ya Arusha, yakilenga kuongeza ufanisi kwenye usimamizi wa utekelezaji wa mabadiliko ya kisera na kimitalaa. Dk Maulid amesema mageuzi ya kweli katika sekta ya elimu hayawezi kupatikana bila kuwa na uongozi bunifu wa kimkakati unaoeleta mabadiliko kama msingi wa maendeleo katika taasisi za elimu. Amesema wakuu wa shule wanapaswa kusimamia mabadiliko kwa kuzingatia matokeo, uwazi katika matumizi ya rasilimali za shule na kujenga utamaduni wa uwajibikaji miongoni mwa walimu na wanafunzi. “Nawasihi mwende kuwa viongozi wenye maono na uwezo wa kufanya maamuzi kimkakati. Muwe pia na ujuzi wa kusimamia mabadiliko ya taasisi mnazosimamia kwa ufanisi kwani ninyi ndio mtakaochochea mabadiko hayo,”amesema. Akizungumza katika hafla hiyo, Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma, Tafiti na Ushauri Elekezi wa ADEM, Dk Lucas Mzelela amesema mafunzo hayo yamelenga kuwawezesha viongozi wa elimu kwa ujuzi wa vitendo, fikra za kimkakati na uwezo wa kusimamia taasisi hizo ili kuleta mabadiliko chanya kwenye sekta ya elimu. Mwenyekiti wa Chama cha Wakuu wa Shule za Sekondari Tanzania (Tahossa), Mkoa wa Arusha Omari Nyangu amesema mafunzo hayo yamekuja wakati muafaka ambao sekta ya elimu inahitaji viongozi wanaoweza kuhimili mabadiliko ya sera, ongezeko la wanafunzi na matarajio makubwa ya jamii. “Maendeleo katika sekta ya elimu hayawezi kupatikana bila uwekezaji katika kuwajengea uwezo viongozi na wasimamizi wa taasisi za elimu. Mafunzo tuliyopatiwa ni dira katika usimamizi wa taasisi za elimu,” amesema Nyangu. Amesema uwekezaji katika kuwajengea uwezo wakuu wa shule ni hatua muhimu ya kuongeza ufanisi wa matumizi ya fedha za umma, hususan katika miradi ya maendeleo ya miundombinu na utoaji wa huduma za msingi shuleni.