WanTam: Upinzani sasa wapima hewa ngome ya Ruto

MUUNGANO wa upinzani chini ya mwavuli wa United Alternative Government, umeanza ziara za mashinani ukilenga kujiimarisha kitaifa kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2027. Mnamo Ijumaa, walianza ziara ya mikutano kaunti ya Nakuru kufuatia mkondo wa mikutano ya siku tatu katika kaunti za Kisii na Nyamira. Muungano huo unawaleta pamoja Fred Matiang'i, Rigathi Gachagua, Kalonzo Musyoka na Eugene Wamalwa. Katika ziara ya Gusii, Matiang’i alipokelewa kwa shamrashamra na hata kuvishwa mavazi ya kitamaduni kama ishara ya baraka za wazee wa jamii, hatua iliyotafsiriwa na wachambuzi kama jaribio la kuimarisha uhalali wake wa kitaifa. Kabla ya mikutano iliyofaulu eneo la Gusii, muungano huo ulifanya mkutano Mulot, Bomet eneo linalochukuliwa kuwa ngome ya Rais William Ruto. Hatua hiyo ilionekana kama jaribio la kupima maji katika maeneo ambayo awali yalikuwa yakiegemea upande wa serikali. Akihutubia wakazi, Wamalwa alinukuu changamoto za gharama ya maisha na ushuru mkubwa, huku Gachagua akiahidi fidia kwa waliotimuliwa katika Msitu wa Mau ndani ya miezi sita iwapo watashinda 2027. “Tutashughulikia ukosefu wa ajira kwa vijana na changamoto za wakulima na wafanyabiashara,” alisema Gachagua. Kwa mujibu wa mchambuzi wa siasa Peter Sitati, ziara hizo zinaashiria mkakati wa mapema wa kuunganisha kura. “Wamegundua kuwa uchaguzi wa 2027 hautakuwa mitandaoni bali mashinani. Swali ni kama wanaweza kudumisha mshikamano wao hadi wakati huo,” alisema. Kulingana naye, ziara hizo ni juhudi za kuondoa taswira ya upinzani kuwa kila mmoja anajipigia debe kivyake. “Wanajaribu kuonyesha kuwa ni serikali mbadala na kufifisha dhana kuwa wao ni makuhani wa siasa za eneo fulani. Muungano huo umesisitiza umuhimu wa uadilifu katika uchaguzi na nia ya kusimamisha mgombea mmoja wa urais. Hata hivyo, historia ya miungano ya upinzani nchini imekuwa ikikumbwa na migogoro ya ndani kadri uchaguzi unavyokaribia. Hata hivyo, kasi ya ziara za upinzani na mapokezi wanayopata inaonyesha kuwa ushindani wa 2027 umeanza mapema. Sitati asema iwapo watafanikiwa kupenya na kudumisha joto hilo mashinani, watahitaji sio tu ajenda inayogusa maisha ya wananchi bali pia umoja wa ndani usiotetereka. “Kwa sasa, dalili zinaonyesha kuwa upinzani umeanza safari ya kujijenga upya lakini kama moto huo utaendelea kuwaka hadi 2027, hilo ndilo swali kuu katika siasa za Kenya,” aeleza. Ziara ya upinzani Nakuru ina uzito wa kipekee kisiasa kwa sababu kaunti hiyo imekuwa ikitazamwa kama mojawapo ya ngome muhimu za Rais William Ruto katika Bonde la Ufa. Katika Uchaguzi Mkuu wa 2022, Dkt Ruto alipata kura nyingi katika kaunti hiyo, Kwa hivyo, kuonekana kwa maelfu ya wakazi wakijitokeza kusikiliza vinara wa upinzani ni ishara yenye ujumbe mzito. Kwanza, inaonyesha kuwa upinzani unajaribu kupenya maeneo ambayo awali yalikuwa yakichukuliwa kuwa ‘bedroom’ kwa serikali. Hii ni mbinu ya mapema ya kuvunja ukuta wa kisaikolojia kwamba baadhi ya maeneo hayawezi kubadilika kisiasa. Pili, mapokezi hayo yanaweza kuwa dalili ya malalamiko ya kiuchumi miongoni mwa wapigakura wa kawaida. Nakuru ni kitovu cha biashara, kilimo na utalii na wachambuzi wanasema huenda ni ishara ya kutaka kusikia sauti mbadala kuhusu gharama ya maisha, ushuru na ajira. Tatu, ni jaribio la kupunguza pengo la kura katika Bonde la Ufa. Hata kama upinzani hautashinda kwa wingi eneo hilo 2027, kupunguza tu tofauti ya kura kunaweza kuwa na athari kubwa kitaifa.