RUTO: Tutashindana na ndugu yangu Oburu kama marafiki 2027

RAIS William Ruto amesema kwamba chama chake cha United Democratic Alliance (UDA) na chama cha Orange Democratic Movement (ODM) vitashindana kama marafiki katika Uchaguzi Mkuu wa 2027, kama sehemu ya juhudi za kuimarisha demokrasia nchini. Rais Ruto alisisitiza ahadi ya Serikali Jumuishi kuendeleza umoja wa kitaifa na usawa katika ugavi wa miradi ya maendeleo kote nchini, akisema kwamba ushindani wa kisiasa kati ya vyama hivyo viwili hautaathiri ushirikiano wao. “Chini ya serikali jumuishi, tumekubaliana kwamba nchi ni muhimu zaidi kuliko chama chochote cha kisiasa, muungano wowote au kiongozi yeyote. Hatuko katika serikali jumuishi kwa sababu ya nyadhifa au maslahi binafsi, bali kwa ajili ya watu wa Kenya,” alisema Dkt Ruto. “Viongozi katika UDA na ODM wana nafasi ya kihistoria kuhakikisha kwamba nchi hii inakuwa na umoja.” Aliongeza: “Mabadiliko ya nchi hii yamecheleweshwa kwa muda mrefu kutokana na mgawanyiko na mawazo madogo.” Rais Ruto alisema hayo jana katika eneo la Mashuru, Kaunti ya Kajiado, wakati wa sherehe kubwa ya shukrani ya chama cha ODM kwa Katibu wa Haki za Binadamu na Masuala ya Katiba, Judy Pareno, iliyoandaliwa licha ya mvua kubwa. Bi Pareno ni mmoja wa viongozi wa ODM walioteuliwa katika nyadhifa mbalimbali za serikali chini ya Serikali Jumuishi. Rais Ruto alisema mazungumzo yanayoendelea kati ya UDA na ODM yatatoa fursa ya ushindani mzuri katika Uchaguzi Mkuu ujao, ambapo kila chama kitaweka wagombea katika viti vyote uchaguzini isipokuwa urais. “Mazungumzo kuhusu makubaliano ya kisiasa kati ya UDA na ODM yako katika hatua za juu. Vyama vitashiriki kwa njia ya kirafiki katika uchaguzi ujao lakini tutaendelea kuwa katika njia moja. Mahali ambapo chama kimoja kitashinda, tutasherehekea pamoja. Tutawakaribisha walioshindwa katika serikali,” alisema Rais Ruto, akiongeza kuwa wapigakura watapata fursa ya kutathmini utekelezaji wa serikali yake mwaka 2027. Rais alikosoa Muungano wa Upinzani, akisema kwamba unaendeleza siasa za mgawanyiko kwa maslahi binafsi badala ya ustawi wa kitaifa.“ODM ya Serikali Jumuishi ni tofauti na wapinzani wetu. Sisi tunaamini katika Umoja wa Kitaifa lakini wao wanajivunia siasa za mgawanyiko na kikabila ambazo hazina nafasi katika jamii ya kisasa,” aliongeza Rais Ruto.