SENETA wa Nandi, Samson Cherargei, amekiri wazi kwamba wanasiasa wengi wa Kenya wanamiliki magenge ya wahuni kama kinga ya kisiasa, na akaitaka Idara ya Uchunguzi wa Jinai (DCI) kuwakamata wote wanaohusika na uhuni kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2027. Seneta huyo alionya kwamba Kenya inakabiliwa na hatari ya kugeuka kuwa "Haiti" ikiwa utamaduni wa kuajiri wahuni hautazimwa mara moja. Cherargei alisema kwamba maafisa wa uchunguzi wa jinai kote nchini wana habari kuhusu wanasiasa wanaomiliki wahuni na kwamba wanaificha kwa malipo ya wanasiasa fulani. “Ukweli ni kwamba wengi wetu wanasiasa, bila kujali mwelekeo wetu wa kisiasa, tunamiliki wahuni kwa ulinzi wetu. Ni mwelekeo hatari ambao umepanuka hadi ngazi ya kaunti kulinda maslahi ya kibinafsi. Ikiwa DCI haitachukua hatua za haraka kuwakamata wanasiasa hawa na wadhamini wao sasa, Kenya ina hatari ya kuwa nchi isiyo na sheria kama Haiti ifikapo 2027,” alisema Seneta Cherargei. Alilaumu pia maafisa wa polisi wa kutoa silaha za serikali kwa watu binafsi wanaotishia amani ya wananchi wa Kenya. Alizungumza katika hafla iliyofanyika Eldoret Jumamosi na akaikosoa DCI kwa "kutaka kupoteza muda" huku ghasia za kisiasa zikiongezeka. Alitaja fujo zilizoshuhudiwa wakati wa mikutano ya Linda Mwananchi katika Kitengela na Kakamega kama dalili ya tatizo kubwa zaidi. "Maafisa wa Uchunguzi wa jinai wanajua wazi kwamba, kama wanasiasa, tunamiliki wahuni, na wamekaa kimya. Kuna wanasiasa wanaovaa mavazi ya kijeshi na silaha haramu. Polisi wanapaswa kuwa wazi ikiwa wanataka tuwe kama Amerika, ambapo kila raia ana haki ya kumiliki silaha anayotaka,” alisema Cherargei. Aliendelea kusema kwamba wanasiasa kutoka pande zote za serikali na upinzani wanamiliki wahuni wanaolipwa kutoa ulinzi, lakini hakufichua ni kiasi gani kila mhuni analipwa. Seneta huyo alitoa mfano wa tukio la kipekee akisema kwamba, “Mwanasiasa mmoja sasa anapigania maisha yake kwenye kitengo cha wagonjwa mahututi (ICU) katika hospitali ya Moi Teaching and Referral Hospital (MTRH) baada ya kushambuliwa na wahuni waliokodishwa Eldoret.” Cherargei alikosoa polisi kwa kutokuchukua hatua dhidi ya wanasiasa wanaovaa sare za polisi hadharani na akataka wanasiasa wote wanaomiliki wahuni na kuvaa mavazi ya polisi hadharani kukamatwa. Alihimiza serikali kuacha wanasiasa wote kufanya mikutano nchini bila kuingiliwa na polisi. Alisema kwamba ikiwa polisi hawatachukua hatua dhidi ya wahuni na kuruhusu wanasiasa kufanya mikutano yao bila usumbufu, nchi iko hatarini kugeuka Haiti. "Mwelekeo wa sasa wa kutumia wahuni ni bomu ambalo linaweza kulipuka wakati wowote. Naomba polisi wa Eldoret kuacha kuzungumza na kuanza kukamata wahusika wote waliohusika katika shambulio la hivi karibuni dhidi ya mwenzetu. Hakuna mtu anaye paswa kuwa juu ya sheria, bila kujali hadhi yake ya kisiasa," aliongeza