TSC yaonya wakuu wa shule wanaoshikilia vyeti vya KCPE na KCSE

TUME ya Kuwaajiri Walimu (TSC) imeagiza wakuu wa shule zote za msingi na sekondari kuachilia mara moja vyeti vya mitihani ya Darasa la Nane (KCPE) na Kidato cha Nne (KCSE) kwa wanafunzi wa zamani, wazazi wao, au walezi. TSC imesema wakuu wa shule watakaokiuka agizo hilo watakachukuliwa hatua za kinidhamu. Agizo hili linafuata malalamishi ya mara kwa mara kutoka kwa wazazi, walezi, wanafunzi na wadau wengine kwamba, baadhi ya wakuu wa shule wamekuwa wakizuia vyeti kwa njia isiyo halali, jambo linalowazuia wanafunzi kuendelea na masomo au kupata ajira. Katika barua kwa wakuu wa shule, TSC ilisisitiza kuwa vyeti vya masomo ni mali ya wanafunzi na haviwezi kutumika kulazimisha ulipaji wa deni la karo. Tume hiyo ilionya kwamba, kushikilia vyeti kunawanyima wanafunzi nafasi za maendeleo kitaaluma na elimu ya juu. “TSC inaendelea kupokea malalamishi kutoka kwa wazazi, walezi, wanafunzi, na wadau wengine kwamba, baadhi ya wakuu wa shule wamekuwa wakizuia kwa njia isiyo halali wanafunzi kupata vyeti vyao vya KCPE na KCSE. Tume hii inaagiza wakuu wote wa shule watoe vyeti vyote vilivyo mikononi mwao mara moja kwa wanafunzi au wazazi/walezi wanaowawakilisha,” alisema Afisa Mkuu Mtendaji wa TSC, Evaleen Mitei. Agizo hili linatarajiwa kuondoa changamoto ya muda mrefu kwa wanafunzi wanaokosa kupata rekodi zao za masomo. Haya yanajiri baada ya Wizara ya Elimu kutoa agizo kama hili mnamo 2025, lakini malalamishi yakaendelea kuwa vyeti bado vinazuiliwa na hivyo kufanya TSC kuandika barua mpya ili kuhakikisha utekelezaji na kulinda haki za wanafunzi. TSC inasema Sheria ya Baraza la Kitaifa la Mitihani Kenya (KNEC) ya 2012 inasema vyeti vitolewe kwa watahiniwa mara tu vinapotolewa, na hakuna mtu au taasisi inayoweza kuvizuia. Aidha, Ibara ya 53 ya Katiba inahakikishia kila mtoto haki ya elimu ikiwemo upatikanaji wa vyeti vyake.