MBUNGE wa Emurua Dikirr Johana Ng’eno aliwajibikia shughuli chungu nzima mnamo Jumamosi asifahamu kuwa hiyo ingekuwa siku yake ya mwisho duniani. Bw Ng’eno na wasafiri wengine watano waliangamia katika ajali ya helikopta eneo la Chepkiep eneobunge la Mosop, Kaunti ya Nandi. Katika mahojiano na Taifa Dijitali, rafikiye mbunge huyo Geoffrey Bett maarufu kama Gechwo alifichua kuwa alipanga kusafiri naye hadi Kaunti ya Trans Nzoia. Alipanga kusafiri kwa helikopta hiyo iliyoanguka msituni Nandi Kaskazini. “Nilikuwa niabiri helikopta hiyo lakini nikawasili dakika tano baada kuchelewa na hivyo ndivyo nimesalia kuishi,” akasema Bw Bett ambaye ni mkazi wa Murkan, eneobunge la Emurua Dikir. Mnamo Ijumaa alikuwa ameandamana na Bw Ng’eno katika hafla mbalimbali kabla ya wawili hao kuagana saa nane usiku na kukubaliana wakutane Jumamosi. Mbunge huyo alimwambia angesafiri Nairobi mnamo Jumamosi asubuhi kisha arudi kwa helikopta kwa hafla za kuwapiga jeki wasanii kaskazini mwa Bonde la Ufa. Hata hivyo, alibadili nia na helikopta ikamchukua nyumbani kwake Mokindo, Emurua Dikir. Awali alifaa kutembelee Trans Nzoia kisha jioni Maria Ranta afuatilie hatua zilizopigwa kuopoa miili ya watu waliokuwa wamezama majini Mto Mara siku tatu zilizopita. Hata hivyo, Bw Bett alimshawishi atembelee Maria Ranta kwanza kisha waende Tran Nzoia. “Nilisafiri kutoka Narok hadi Changina kule Ainamoi, wadi ya Elkerin ambako Bw Ng’eno alikuwa na hafla mnamo Ijumaa. Aliniuliza kuhusu kusakwa kwa miili ya waliokufa maji na nikamwaambia hawajapatikana ndipo akasema atatembelea eneo la tukio mwenyewe Jumamosi,” akakumbuka. Mnamo Jumamosi, Bw Bett alimpigia Bw Ng’eno kuthibitisha mahali ambapo wangekutana na kama alisafiri Nairobi lakini simu yake haikuwa ikiingia. “Saa sita na dakika nne nilimpata lakini nilichelewa kwa sababu helikopta ilikuwa tayari nyumbani kwake na angenichukua tu Mara Rianta. Bw Bett alichukua bodaboda lakini akafika Mara Rianta kama helikopta ilishaenda hii ni kwa sababu pikipiki aliyokuwa ameabiri ilitoboka kwenye gurudumu. Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu wa Shule za Upili nchini tawi la Kilgoris Willy Korir alisema mbunge huyo alitoa hundi za basari Mogindo kabla ya kuondoka kwa helikopta. “Alisema ilikuwa mara yake ya kwanza kutumia helikopta hiyo na hakufamu rubani. Hakuna aliyejua hiyo ndiyo ilikuwa mara ya mwisho kumwona,” akasema Bw Korir. Saa kadhaa kabla ya mauti yake, mbunge huyo alikuwa amesafiri Kapkugo, Tulwop Kony na Endebes, akijiunga na wenyeji na wakazi kuadhimisha miaka 35 ya usanii wa Kim Kim kwenye fani ya burudani.