URAFIKI mpya wa kisiasa kati ya Waziri wa Madini, Bw Hassan Joho na Mbunge wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA), Bw Suleiman Shahbal, umeashiria mwelekeo mpya ambao unaweza kubadilisha kinyang’anyiro cha ugavana Mombasa mwaka wa 2027. Kwa wiki kadha sasa, Bw Joho amekuwa akionekana bega kwa bega na Bw Shahbal katika hafla mbalimbali, ishara ya mikakati inayopangwa kuelekea 2027. Wawili hao wamehudhuria hafla kadhaa pamoja, zikiwemo za eneo la Kaskazini Mashariki, Lamu, Tana River na maeneo mengine mbali na Mombasa. Hata hivyo, madhumuni yao halisi yalibainika wazi Jumamosi, Februari 28, pale Bw Joho alipotangaza wazi kumuunga mkono mfanyabiashara huyo, ambaye atawania kiti cha ugavana kwa mara ya tatu. “Wakati huu, nataka kuwaambia kwamba ikiwa Bw Shahbal ameamua, nami pia nimeamua. Ni msemaji mzuri, ana rasilimali, ni mjanja na ana uzoefu wa kisiasa,” alisema Bw Joho. Jumamosi usiku, wawili hao walihudhuria hafla ya kuchangisha fedha kwa ajili ya Klabu ya Soka ya Mombasa United, iliyoanzishwa na Bw Shahbal mwaka 2021 wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu. Bw Joho na ndugu yake Abu Joho hadi sasa wamekuwa wakimuunga mkono rafiki yao wa muda mrefu, Gavana Abdulswamad Nassir. Ndugu hao wawili wana ushawishi mkubwa katika siasa za Mombasa. Mnamo 2022, Bw Shahbal alishawishiwa na viongozi wa ODM wakiongozwa na marehemu Raila Odinga kujiondoa katika kinyang’anyiro cha ugavana kumuunga mkono Bw Nassir. Pendekezo hilo liliungwa mkono na rais mstaafu Uhuru Kenyatta aliyekuwa kinara mwenza wa muungano wa Azimio. Baada ya kuwa wapinzani wa kisiasa katika chaguzi zilizopita za ugavana, maridhiano kati ya Joho na Shahbal yanaashiria mpangilio mpana upya wa miungano huku wanasiasa wa eneo hilo wakipanga mikakati kuelekea 2027. Katika mahojiano ya hivi majuzi na Taifa Dijitali , Bw Shahbal alifichua kuwa atawania tena wadhifa huo. “Kwa nini isiwe hivyo?” alihoji alipobanwa atangaze msimamo kuhusu malengo yake ya kisiasa. Baadaye alikutana na wataalamu wa jamii ya Waluo mjini Mombasa, ambapo alitangaza hadharani azma yake. Pia aliwaomba wapigakura wa Mombasa wamsamehe kwa kujiondoa katika kinyang’anyiro cha 2022 na kumuunga mkono Bw Nassir. Alidai aliitwa Nairobi na wakuu wa chama akiwemo Bw Joho, kisha aliarifiwa kuwa umaarufu wake ulikuwa asilimia 45, nyuma ya mpinzani wake, licha ya kufanya utafiti binafsi uliomwonyesha akiongoza kwa asilimia 22. Mfanyabiashara huyo alisema Bw Odinga alimwambia kuwa taifa ni kubwa kuliko azma yake binafsi. Bw Shahbal alieleza kuwa alijikuta katika njia panda baada ya kuzungumza pia na Rais Kenyatta. “Shinikizo nililopitia analijua Mungu pekee. Lakini tuyaache yaliyopita na tuangalie yajayo,” alisema. Ushindani wa kumrithi Gavana Nassir, anayehudumu muhula wake wa kwanza, umepamba moto huku kampeni za mapema zikisitishwa kwa muda tu mwezi huu kutokana na Ramadhani. Gavana huyo anategemea kuchaguliwa tena akitaja mchango wake katika sekta za elimu, afya, maji na usafi wa mazingira miongoni mwa mengine. Hata hivyo, wakosoaji wake wanasema sekta nyingi muhimu zimezorota chini ya uongozi wake, huku wafanyabiashara na wakazi wakilalamikia ongezeko la ada mbalimbali za kaunti. Katika chama tawala cha UDA, aliyekuwa Mbunge wa Kisauni Ali Mbogo anatarajiwa kuwania tiketi dhidi ya Katibu Mkuu Hassan Omar. Upande wa upinzani ukiongozwa na aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua na kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka, umemtangaza Mbunge wa Nyali Mohamed Ali kuwa mgombea wao. Mbunge huyo ndiye pekee wa UDA mjini Mombasa, ambapo wabunge wengine watano, Seneta, Mbunge Mwakilishi wa Kike na Madiwani wengi ni wanachama wa ODM.