Jinsi Ng’eno aliwaokoa Kanja na DCI dhidi ya umati wenye hasira Angata Barikoi

WAKAZI wa Angata Barikoi wamesimulia jinsi maafisa wakuu wa usalama na wanasiasa walivyolazimika kukaa ndani ya helikopta zao baada ya umma kukataa mkutano kuendelea hadi Mbunge wa Emurua Dikirr, Yohana Ng’eno, alipowasili na kugeuza hasira kuwa majadiliano. Jumanne, Aprili 29, 2025, Inspekta Jenerali wa Polisi, Douglas Kanja na Mkurugenzi wa Uchunguzi wa Uhalifu (DCI), Mohamed Amin waliwasili Angata Barikoi Transmara Kusini, Kaunti ya Narok, kwa mkutano wa kujadili amani. Bw Kanja aliongoza kundi la maafisa wakuu wa usalama katika eneo hilo lililoathiriwa na machafuko kwa siku kadhaa ambapo watu sita, akiwemo mtoto wa umri wa miaka sita, waliuawa kwa risasi zilizoripotiwa kufyatuliwa na polisi. Ghasia hizo zilizuka baada ya msafara wa maafisa wa kikosi cha GSU na Wizara ya Ardhi ulipojaribu kuendeleza mchakato wa ugavi wa ardhi katika sehemu ya Moyoi. Wengi walidai kuwa ardhi husika ilielekea kunyakuliwa na watu wenye ushawishi mkubwa wanaohudumu katika serikali inayotawala ya Kenya Kwanza, madai yaliyozidisha shaka na kuchochea hamaki. Katika juhudi za kuzuia umwagikaji damu zaidi, Bw Kanja aliitisha mazungumzo na watu wa Angata Bariko akitumai kusikiza malalamishi na kuwezesha amani ua kudumu. Helikopta ya polisi iliyowasafirisha Bw Kanja na Amin ilitua kwenye uwanja wa Shule ya Msingi ya Angata ambapo mamia ya wakazi walikusanyika. Awali, Kiongozi wa Wengi katika Seneti, Aaron Cheruiyot, aliyekuwa gavana wa Bomet, Isaac Ruto na Mbunge wa Belgut, Nelson Koech, walikuwa vilevile wamewasili Angata kwa kutumia helikopta. Hata hivyo, Bw Kanja na msafara wake walipotua, walikumbana na mazingira yaliyotanda taharuki, ambapo wakazi waliwafukuza maafisa wa GSU waliotumwa kulinda usalama eneo hilo wingu la majonzi na ghadhabu likigubika uwanja huo wa shule. Bw Kanja na Amin walitazama huku wakazi wakiwakabili Bw Cheruiyot na viongozi wengine, wakisisitiza hakuna mkutano utakaoendelea bila mbunge wao, Bw Ng’eno, aliyesimama nao wakati wa ghasia za kikatili. Maji yalipozidi unga, Bw Kanja na Bw Amin waliabiri tena helikopta na kusalia ndani kwa karibu saa moja huku majadiliano yakiendelea nje. “Bw Kanja alikuja bila Bw Ng’eno wetu. Hatungemruhusu kufanya mkutano bila mbunge wetu jasiri, ambaye siku iliyotangulia alikuwa nasi polisi walipotufyatulia risasi. Tuliitisha kuwepo kwake kabla ya mkutano wowote wa usalama kufanyika,” alisimulia Johana Kiprono almaarufu Kamilan, mwanaharakati mashuhuri Transmara Kusini. Helikopta iliyomsafirisha Bw Ng’eno ilipotua hatimaye kwenye uwanja wa Shule ya Angata, mamia ya wakazi waliosubiri tangu asubuhi walisonga mbele na kumbeba mabegani. Hapo ndipo Bw Kanja na kikosi chake waliruhusiwa kushuka ndege tena na mkutano uliosubiriwa kwa muda mrefu ukaanza.