Urafiki tata baina ya Ng’eno, Ruto na Rigathi

MASWALI yameibuka kuhusu msimamo wa kisiasa wa Mbunge wa Emurua Dikirr, Johana Ng’eno ambaye aliaga dunia mnamo Jumamosi katika ajali ya helikopta. Hii ni baada ya aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua kutoa madai yaliyoashiria alikuwa na uhusiano wa karibu wa kisiasa na mbunge huyo aliyekuwa akihudumu muhula wake wa tatu. Kwa upande mwingine, viongozi wa Kusini mwa Bonde la Ufa ambao ni wandani wa Rais William Ruto walimwomboleza Bw Ng’eno na kuashiria alikuwa katika mrengo wa serikali. Bw Ng’eno pamoja na watu wengine watano waliaga dunia katika ajali ya helikopta katika msitu wa Nandi Kaskazini, Kaunti ya Nandi mnamo Jumamosi. Bw Gachagua mnamo Jumapili alitaka uchunguzi zaidi ufanywe kuhusu kilichosababisha kifo cha Bw Ng’eno “ili ukweli ujulikane”. Alizua kumbukumbu jinsi alivyokutana na Bw Ng’eno katika hoteli moja jijini Kisumu kabla ya kutimuliwa kwake ambapo ni mbunge huyo aliyemfichulia mpango uliokuwa ukisukwa wa kumng’oa madarakani. “Wakati huo majasusi wa serikali walitumiwa kurekodi mazungumzo yangu na Johana Ng’eno. Alitishiwa kila mara baada ya tukio hilo,” akasema Bw Gachagua. Kiongozi huyo wa DCP vilevile alisema kuwa ni mbunge huyo aliyemwalika wiki jana ili azungumze na wakazi wa Bomet na Kusini mwa Bonde la Ufa wakati vinara wa upinzani walikuwa wakielekea ziara ya siku tatu eneo la Gusii. Ni wakati wa hotuba katika maeneo mbalimbali Kusini mwa Bonde la Ufa ambapo Bw Gachagua alidai kuwa Rais Ruto amelitelekeza eneo hilo kisiasa . Bw Gachagua amependekeza kuwa uchunguzi huo ufanywe na kikosi cha FBI au kile cha Scotland Yard, vikosi ambavyo ni maarufu sana katika kuchunguza vifo tata. “Murkomen amekuwa akipigana na Ng’eno na tunataka Ruto amwambie ajiondoe ili uchunguzi huo uendeshwe na Scotland Yard au FBI,” akasema Bw Gachagua. Pia alidai kulikuwa na wanasiasa ambao walikuwa wakipinga Bw Ng’eno kuwa msemaji wa jamii ya Kipsigis. Kinaya ni kwamba mbunge huyo alikuwa kati ya wale waliounga hoja ya kumbandua Bw Gachagua. Rais Ruto jana alimtembelea familia ya Bw Ng’eno na hata kumrejelea kama rafiki yake huku akisema mbunge huyo alipenda mno muziki. “Ng’eno alipenda sana muziki na mara kwa mara alikuwa akiniambia mambo ya wasanii,” akasema Rais akikumbuka mbunge huyo aliwahi kumwomba Sh20 milioni ili kuwatunuku wasanii katika mashindano aliyokuwa ameandaa. “Najua kile Ngéno alisi mamia na najua jinsi tukio hili sasa limefanya wakazi wa Emurua Dikirr wahisi vibaya kwa sababu Ngéno alipenda sana kile alichofanya,” akaongeza Rais Ruto. Hasa Rais alisema mbunge huyo alikuwa akitekeleza wajibu muhimu katika mradi wa ujenzi wa nyumba za gharama nafuu hasa akiwa mwenyekiti wa kamati ya nyumba na makao bungeni.