Seneti yaibuka na mbinu ya kukabili magavana wanaokaidi vikao vya PAC

BUNGE la Seneti sasa litawaamrisha magavana ambao wamekataa kufika mbele ya Kamati ya Uhasibu Seneti (PAC) waadhibiwe kwa kutozwa faini au kukamatwa. Hatua hiyo inakuja wakati ambapo kuna uhasama kati ya Seneti na Baraza la Magavana Nchini (COG) kuhusu madai ya hongo dhidi ya PAC. COG mwezi uliopita iliandaa kikao na wanahabari na kutangaza kuwa wanachama wake hawatakuwa wakifika mbele ya PAC kwa sababu baadhi ya maseneta wamekuwa wakiwaitisha hongo. Walienda hatua moja mbele na hata kuorodhesha majina ya baadhi ya maseneta hao. Tayari magavana wanne wamefuata amri ya COG na kukosa kufika mbele ya PAC. Kutokana na kile ambacho kinaonekana kama mchezo wa paka na panya, baadhi ya magavana waliandikia PAC barua kuhusu kutopatikana kwao. Gavana wa Kisii Simba Arati kwa mfano, alitangaza kuwa hayupo nchini na akaomba kikao cha kufika mbele ya kamati hiyo kiahirishwe hadi mwisho wa mwezi huu. Kinaya ni kwamba kamati hiyo inayoongozwa na Seneta wa Homa Bay Moses Kajwang’ ina hadi Machi 31, 2026 kutathmini ripoti ya ukaguzi, kuandaa ripoti yake na kuiwasilisha mbele ya seneti. Gavana wa Kericho Erick Mutai aliomba muda zaidi kumwezesha kujiandaa huku Gavana wa Kajiado Joseph Ole Lenku akisema hangeweza kufika mbele ya kamati hiyo kwa sababu ya shughuli zilizopangwa mapema zilizomlazimu kusafiri nje ya nchi. Gavana wa Kakamega Fernandes Barasa naye alisema hangeweza kupatikana kwa sababu ambazo haziwezi kuepukika lakini hakutaja sababu hizo. Magavana wa kaunti za Kisii na Kajiado walikuwa wafike mbele ya PAC mnamo Jumatatu kisha Kericho na Kakamega siku ya Jumanne (leo). Wiki jana, Gavana wa Nyamira Amos Nyaribo alifika mbele ya kamati hiyo lakini baada ya dakika chache, akasema anahisi kuugua sana wala hawezi kuendelea na mkutano huo. Kilichowashangaza wengi ni kwamba alikataa pendekezo la kupelekwa hospitalini iwapo alikuwa katika hali hiyo mbaya kiafya. Kwa wiki ya tatu bila kikao, kamati hiyo sasa imeamua kuwa kila gavana ambaye atakaidi kufika mbele yake lazima aadhibiwe kwa faini ya Sh500,000 au kukamatwa kupitia amri ya Inspekta Jenerali Douglas Kanja. “Tumepokea barua zinazoomba vikao vya Jumatatu na Jumanne viahirishwe hadi wiki ijayo. Mwenyekiti amewaamrisha magavana hao wafike mbele ya kamati hii haraka muda wowote ambao utapatikana mapema,” ikasema waraka ulioandikiwa kamati. Wiki jana COG ilisema magavana hawawezi kufika mbele ya PAC baada ya mkutano wao wa upatanishi na Spika wa Seneti kugonga mwamba. Mwenyekiti wa COG Ahmed Abdullahi alisema kuwa magavana watafika mbele ya kamati nyingine za Seneti ila si PAC hadi masuala waliyoyaibua yasuluhishwe.