Iran yaapa kushambulia meli zinazopita Mkondo wa Hormuz

TEHRAN, IRAN KAMANDA mmoja katika Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi cha Iran (IRGC) amesema Mkondo-Bahari wa Hormuz umefungwa na kuonya kwamba chombo chochote kitakachojaribu kupita eneo hilo kitashambuliwa. "Mkondo wa Hormuz umefungwa. Ikiwa mtu yeyote atajaribu kupitia hapo, mashujaa wa Walinzi wa Mapinduzi na jeshi la majini watateketeza meli hizo," Ebrahim Jabari, mshauri mkuu wa kamanda mkuu wa IRGC, alisema. Haya yanajiri huku Tehran ikilenga miundombinu muhimu wa kuzalisha nishati duniani kama sehemu ya kulipiza kisasi kwa mashambulizi ya Israeli na Amerika iliyoanza Jumamosi na kusababisha kifo cha Kiongozi Mkuu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei na maafisa wengine wakuu. "Pia tutashambulia mabomba ya mafuta na hatutaruhusu hata tone la mafuta kuondoka katika eneo hilo. Bei ya mafuta lita moja itafikia Sh25, 800 katika siku zijazo," Jabbari alisema katika chapisho kwenye mtandao wa Telegram ya IRGC. "Wamarekani, wenye madeni ya maelfu ya mabilioni ya dola, wanategemea mafuta ya eneo hilo, lakini wanapaswa kujua kwamba hata tone la mafuta halitawafikia," aliongeza. Mkondo wa Hormuz, ambao uko kati ya Iran na Oman, ni mojawapo ya njia muhimu zaidi za usafirishaji wa mafuta duniani, huku takriban asilimia 20 ya usambazaji wa mafuta duniani ukipitia humo. Hatua hiyo itaathiri pakubwa bei ya mafuta duniani. Tayari bei ya gesi asilia, imepanda kwa karibu asilimia 50 barani Ulaya na karibu asilimia 40 barani Asia huku QatarEnergy, muuzaji mkuu, ikisimamisha uzalishaji wake baada ya vifaa vyake vya LNG kushambuliwa. Amerika ilisema itachukua hatua kupunguza kupanda kwa bei za nishati kutokana na vita kati yake na Iran, kulingana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Amerika Marco Rubio. “Tulijua bei ingepanda hivyo tutachukua hatua haraka iwezekanavyo kuhakikisha bei inakuwa sawa,” Rubio alisema. Siku ya Jumatatu Machi 02, pipa moja la mafuta lilikuwa likiuzwa Sh10, 582 ambayo ni ongezeko la asilimia 13 ikilinganishwa na bei ya wiki iliyopita. Shirika la Umoja wa Mataifa la Usafiri wa Anga lenye makao yake mjini Montreal, Canada, limesema mataifa duniani yana wajibu wa kuhakikisha usalama wa safari za ndege ili kupunguza hasara inayoshuhudiwa. Huku nchi hizo zikiendelea na mashambulizi, Iran jana ililenga ubalozi wa Amerika nchini Saudi Arabia. Wizara ya Ulinzi ya Saudi Arabia imesema ndege mbili zisizo na rubani zimeushambulia ubalozi huo mjini Riyadh. Rais Donald Trump ameapa kulipiza kisasi kwa uamuzi wake wa kuushambulia ubalozi wa nchi yake na kwa mauaji ya wanajeshi 6 wa Amerika tangu kuanza kwa vita Jumamosi iliyopita. Nchi zilizoathirika na mashambulio hayo ni Bahrain na Kuwait.