KADRI nafasi za ajira za afisini zinavyozidi kuadimika humu nchini, Wakenya wengi hasa vijana wanajizatiti kuhakikisha wanazamia ufugaji kama njia moja ya kujizolea riziki yao ya kila siku. Katika Kaunti ya Nyamira, Rashid Mohamed,34, amewekeza katika ufugaji wa aina mbalimbali za ndege. Mfugaji huyu aliyeupenda ufugaji tangia siku zake alipokuwa akisoma katika shule ya wavulana ya Kisii High, ni mfugaji hodari wa ndege mbalimbali, lakini tulivutiwa na ufugaji wa bata bukini. Jarida la Akilimali lilipata fursa ya kutangamana na Rashid nyumbani kwao kijijini Keboba, Gachuba kwenye eneobunge la Kitutu Masaba, mpakani mwa kaunti za Kisii na Nyamira. Mandhari mazuri ya eneo tambarare yalitukaribisha kijijini humo, takribani kilomita tatu kutoka mji wa Keumbu. Rashid anayemiliki bata bukini zaidi ya 100 wa sampuli tofauti alieleza tija inayopatikana katika ufugaji wa ndege hao. Pia ana kuku wengine wa mapambo kama vile silkies, walio na manyoya mithili ya sungura. “Bata bukini ni mojawapo ya ndege ambao mkulima anaweza kuwamudu kuwalinda kwa gharama ndogo ikilinganishwa na ndege wengine kama vile kuku. Bata bukini, wanapatikana kwenye familia moja na bata wa kawaida,” alisema Rashid. Bata bukini ni wakubwa kwa kimo, rangi yao ni nyeupe au kijivu na wengine wana mabaka meupe na meusi. Aidha wao hushamiri vyema katika maeneo yenye baridi kali hususan nyanda za juu. “Nchini Kenya, bata bukini hufugwa kwa wingi katika ukanda wa Bonde la Ufa na eneo la Kati. Kwa kuwa hali ya anga huku Gusii ni sawia na maeneo hayo, niliamua kuwazamia pia,” Rashid anaeleza. Yeye ni mhandisi kitaaluma. Hamu yake ya ufugaji aliipata alipokuwa katika shule ya upili. Kwa wakati huo, alikuwa na bata bukini wachache tu, ambao alikuwa amewaachia wazazi wake wamtunzie. Alipomaliza masomo yake, alipanua mradi wake na kuwa na bata bukini zaidi ya 100. Alipata kibarua jijini Nairobi na hilo likamlazimu awaachie mtu kibarua cha kumtunzia ndege hao. Lakini aliporejea nyumbani wakati wa likizo yake, alipata kuwa mradi wake ulikuwa unadidimia. Alichukua hatua ambayo ni nadra kwa wengi kuichukua; kuachana na kazi hiyo na kurejea kijijini Keboba ili kuufufua mradi wake. Kufikia sasa, Rashid ana ndege mbali mbali nyumbani kwao. Ndege hawa wanahusisha kuku wa kawaida, njiwa, ndege wa mapambo na bata bukini wapatao zaidi ya 100. Anasema siri ya kuwatunza bata bukini ni kuelewa ulaji wao, mazingira wanamokulia, mahitaji ya soko na jinsi ya kukabiliana na mkurupuko wa maradhi. Pili, anawahimiza vijana kujipatia ujuzi wa kufanya ukulima, ili kuyaboresha maisha yao, katika ulimwengu wa sasa ambapo nafasi za ajira ni finyu. Rashid alihoji kuwa ni muhimu sana kwa mfugaji kutoa viwango sahihi vya lishe kwa bata bukini, ndege wa kigeni ambao wamekulia sana bara Asia. “Wakati mwingi chakula chao kinahitaji kuchanganywa na nafaka zilizosagwa, maji ya kutosha na kuwaweka ndani ya mazingira safi,” alisema Rashid. Alieleza kuwa wakati wa kuwafuga, mkulima anahitaji kuwawekea bwawa la maji, hususan idadi yao ikiwa kubwa, ili kuwapumbaza dhidi ya kuzurura katika mazingira jirani ikiwa mkulima hajazungusha ua katika boma lake. Lakini kwa kuwa hataki ugomvi na majirani, Rashid amezungusha ua katika boma lake ili kuwazui kuzurura kwenda kwa majirani anapowafungulia. Hatua hii imemsaidia kuepuka ugomvi na majirani wake. Pia anadokeza kuwa kuwazungushia ua la kuwazuia kuzurura huwaepushia ndege hao hatari ya kupata maradhi ya kuambukizana, ama hasara ya kupotea wanapokosa mwelekeo wa kurudi nyumbani. Ndege hawa wenye milio kama firimbi wana rangi ya kuvutia, hupenda kuogelea na mara nyingi hujipanga wawili wawili wakitafuta sehemu ya kutaga mayai. Kulingana na Rashid, bata bukini wana hekima nyingi hasa kwenye suala la kukabiliana na adui. Yeyote anapoingilia mazingira yao na kuwachokoza ama kuiba mayai hana budi kukabiliana nao. “Huweka ulinzi mkali na kuwafurusha wageni wapya wanaozuru makazi yao, na wakati wa kuangua dume ndio huyalinda mayai,” anasema. Ingawa malezi yao ni kama kuku wa kawaida, mayai huangua baada ya wiki tatu takriban siku 21 tangu wayatamie mayai. Bata bukini hutaga kati ya mayai 6-8 kutegemea na mazingira wanamokulia na utulivu wa akili wanaopata. Purukushani na kelele kutoka kwenye sauti za magari au viwanda hukata uwezo wao kutaga mayai kwa wingi. Kulingana na mkulima huyu, bata jike ndiye hutoa matunzo kwa vifaranga anapowazingira wa mabawa yake na kuwapatia joto. Vifaranga huchukua kati ya miezi 2-3 kukomaa ndipo wakaanza kutembea japo kwa kuyumbayumba, kabla ya kupata nguvu, kwenye miguu wakasimama tisti. Kwa mwezi mzuri, Rashid anaweza kupata angalau Sh50,000 kutokana na biashara ya bata bukini. Fedha hizi hutokana na uuzaji wa mayai na hata ndege wenyewe.