Spika Zungu aahidi mazingira bora ya kisheria kwa wanawake

Dar es Salaam. Spika wa Bunge la Tanzania, Mussa Azzan Zungu ameahidi kuwa Bunge litakuwa mdau wa kwanza katika kuhamasisha mazingira bora ya kisheria yanayochochea usawa wa kijinsia nchini na kuwainua wanawake. Spika Zungu ametoa ahadi hiyo leo Machi 4, 2026 wakati wa hafla ya wahitimu wa mafunzo ya wanawake na uongozi awamu ya 11, yaliyofanyika jijini Dar es Salaam. Katika sherehe hiyo, wafanyakazi 158 kutoka taasisi na kampuni mbalimbali nchini wamehitimu mafunzo hayo yaliyoandaliwa na Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) pamoja na chuo cha mafunzo cha Esami na Serikali ya Norway. Akizungumza kwenye hafla hiyo, Zungu amewahakikishia wadau kwamba Bunge litaendelea kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi kwa kuzingatia haki za wanawake ambao kihistoria wanaachwa nyuma kutokana na kushamiri kwa mfumo dume katika jamii. "Niwahakikishie kwamba Bunge litakuwa mdau wa kwanza katika kujenga mazingira bora ya kisheria kwa wanawake, kwani wamethibitisha kwamba wana uwezo na uwezo wao unalinufaisha Taifa kwa ujumla," amesema Zungu. Mbali na hilo, Spika Zungu amewataka wanawake kupendana ili wafike mbali kwani uzoefu unaonyesha wanashindwa kupiga hatua kwa sababu ya chuki miongoni mwao, jambo linalowarudisha nyuma. "Wanawake mnasemana sana, mnasengenyana, mtu akipendeza tu, anasemwa. Niwaombe sana mpendane, mkipendana na kushikamana mtafika mbali sana," amesema kiongozi huyo wa Bunge. Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa ATE, Suzan Ndomba-Doran amesema taasisi yake iliyaleta mafunzo ya uongozi kwa wanawake kutoka Norway kwa lengo la kuwajenga kiuongozi na kuwafungulia fursa zilizo mbele yao. Katika mafunzo ya mwaka huu, amesema jumla ya wafanyakazi wanawake 158 wamehitimu mafunzo hayo na kufanya jumla ya wanawake walionufaika na.mafunzo tangu mwaka 2016 kufikia 803. "Tunatambua mchango wa waajiri katika kufanikisha mafunzo haya kwa kuwaruhusu na kuwafadhili ili washiriki, tunawapongeza na kuwashukuru sana waajiri hapa nchini," amesema Suzan. Ameongeza kuwa mwaka huu, taasisi 21 zimepeleka wafanyakazi wao kwenye mafunzo hayo ambapo idadi ya wahitimu imekuwa ikiongezeka siku hadi siku, na kuwafanya wanawake kuwa bora zaidi katika taasisi zao. Mwakilishi wa kampuni ya Vodacom Tanzania, Hilda Bujiku amesema zaidi ya wafanyakazi wanawake 50 wa Vodacom wamepata mafunzo hayo tangu yalipoanza mwaka 2016. Amesema hadi sasa wanawake katika kampuni hiyo ni asilimia 45, jambo ambalo limechochewa na utashi wa kampuni yenyewe na kutokana na mafunzo hayo, wanaona thamani ya uwekezaji wao katika kuwawezesha wanawake. "Wito wangu kwenu, tengenezeni wanawake wengine, kila mmoja wenu amwinue mwanamke mwingine. Mkifanya hivyo, hapo ndipo mabadiliko yanapoanzia," amesema Bujiku kutoka Vodacom. Naye, mwakilishi wa wahitimu wa awamu ya 11, Magaline Magali amesema wanawashukuru waajiri kwa kuamini katika nguvu ya wanawake na kuwekeza kwao katika mafunzo hayo na bila shaka watapata manufaa ya uwekezaji wao wa mwaka mzima. "Mafunzo yetu yalikuwa ni zaidi ya darasani, tulitembelea sehemu mbalimbali kama JKCI ambako tulichangia Sh30 milioni ili kuwasaidia watoto wanaohitaji matibabu ya moyo. "Tulipowaona wale watoto, tuliendelea kujipapasa, tuliongeza mchango wetu hadi kufikia 35 milioni, tunaomba utufikishie salamu zetu kwa bodi," amesema mhitimu huyo, akiwasilisha ombi kwa Zungu.