ALIYEKUWA waziri Raphael Tuju na watoto wake watatu, wametozwa faini ya Sh100,000 kila mmoja kwa kukiuka maagizo ya mahakama, katika mzozo wa kisheria unaohusiana na uongozi wa kampuni ya Dari Limited, iliyokuwa ikifanya kazi kama mkahawa mtaani Karen, Nairobi. Mahakama Kuu ilisema kwamba Tuju pamoja na Mano Tuju, Alma Tuju na Yma Tuju, walikiuka kwa makusudi maagizo yaliyotolewa Machi 2 na Machi 13, 2020. Mahakama ilikataa maombi yao ya kufutilia mbali hukumu iliyotoa Julai 2020 iliyowapata na hatia ya kudharau korti. Mahakama ilikuwa imewaagiza kuruhusu meneja mrasimu aliyeteuliwa na mahakama katika ofisi za Dari Limited na kuhakikisha wanapata rekodi zake zote ili kurahisisha usimamizi wa kampuni. Hata hivyo, mameneja hao waliripoti kuwa walizuiwa mara kwa mara kuingia katika ofisi za kampuni. Mahakama iliwapa siku 90 kulipa faini hiz la sivyo wafungwe jela miezi sita. Mahakama ilisema kuwa familia ya Tuju haikuweza kutoa sababu halali za kukiuka maagizo ya korti ya Machi 2020 katika mzozo wa uongozi kati ya Dari Limited na Benki ya Maendeleo ya Afrika Mashariki (EADB). Mzozo ulianza mwaka 2019 kutokana na kesi ya kibiashara kati ya Dari Limited na S.A.M Company Limited, zote zinazohusishwa na Tuju, dhidi ya EADB. Mgogoro ulitokana na mkopo wa dola 9.3 milioni uliotolewa kwa Dari Limited na EADB kwa mradi wa makazi mtaani Karen. Baada ya kukosa kulipa mkopo mwaka 2017, Benki ilianza mchakato wa kurejesha deni hilo, ambalo lilifikia takribani Sh1.6 bilioni pamoja na riba. Mnamo Desemba 2019, EADB iliwateua meneja mrasimu Muniu Thoithi na George Weru kusimamia mali ya Dari Limited. Tuju alikata rufaa mahakamani, na kuanzisha mzozo wa kisheria kuhusu uongozi wa kampuni. Rekodi zinaonyesha kuwa Machi 2020, mahakama iliruhusu meneja mrasimu kuingia ofisi na rekodi za Dari Limited ili kurahisisha urejeshaji wa deni. Hata hivyo, meneja aliripoti alizuiwa mara kwa mara, licha ya maagizo ya mahakama. Mnamo Julai 2020, Mahakama Kuu ilipata Tuju na wanawa na na hatia ya kukiuka maagizo ya mahakama kwa makusudi.