JUMA lililopita tuliangazia kwa kina uandishi wa insha ya ripoti. Juma hili tutaanza kuangalia uandishi wa insha ya tahariri. Tahariri ni insha ambayo huandikwa na mhariri wa gazeti kwa madhumuni ya kutoa mwelekeo fulani unaohakiki jambo linaloathiri jamii pana. Tahariri huonyesha msimamo wa mhariri au wa gazeti kuhusu jambo linalozungumziwa. Baadhi ya tahariri hujadili pande mbili za jambo moja bila kutoa msimamo kwa madhumuni ya kuweka jambo fulani wazi. Tahariri kimsingi huandikwa magazetini ama ikasomwa kwenye vyombo vya habari kama vile redio au runinga. Kichwa Kichwa cha tahariri huonyesha jina la gazeti lenyewe au kituo cha habari. Kichwa pia huwa na tarehe ambayo tahariri hiyo iliandikwa. Utangulizi Utangulizi wa tahariri kimsingi hufafanua zaidi kuhusu mada. Aya ya kwanza ndiyo hujumuisha utangulizi huo. Mwili Mwili wa tahariri hubeba maudhui ya suala linalojadiliwa. Maelezo yote yanayotolewa kuhusiana na mada husika hupangwa kwenye aya. Kila hoja ama maudhui hupewa aya yake. Kila hoja hujadiliwa kwa kina kwa kutolewa sababu na ithibati za kutosha. Iwapo suala litakuwa na pande mbili, pande zote lazima ziangaziwe kisha kuibuka na hoja nzito zenye ukweli usiopingika. Hoja zitetewe na kutolewa mifano, takwimu na ithibati mbalimbali. Mhariri anaweza kutoa maoni yake katika tahariri, muradi tu yawe yanatoa ufafanuzi zaidi kuhusu mada anayozungumzia. Hata hivyo, maoni hayo yasiwe ya uchochezi. Lugha ya kushawishi itumiwe katika kuwasilisha hoja na mawazo ya mwandishi. Mwandishi pia ana uhuru wa kujumuisha hisia zake kwenye tahariri. Kwa mfano anapozungumzia maafa, toni za masikitiko au huzuni zinaweza kujitokeza. Msimamo dhabiti huchukuliwa wakati wa kuwasilisha hoja, japo kwa kudumisha maadili ya kitaaluma. Ijapokuwa tahariri huwa na uzito wa kufikirisha, mwandishi anaweza pia kuburudisha hadhira yake kwa kuwasilisha ujumbe wake kwa kudhihirisha umilisi wa lugha ambayo lazima ijikite katika uhalisia wa mambo na isionyeshe porojo. Tahariri huchochea watu kufikiria na kuchukua mitazamo tofauti kuhusu jambo fulani. Ikumbukwe kuwa tahariri hubeba jina la kampuni au la gazeti, majina ya wahariri na vyeo vyao katika hitimisho.